Wajumbe wa mkutano wa IV Kimataifa kujadili kuhusu mtoto kama mtu na mgonjwa mjini
Vatican!
Mfuko wa Msamaria mwema, Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi
katika sekta ya afya, kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 15 Juni 2013 utaendesha mkutano
wa nne wa kimataifa unaojadili kuhusu "mtoto kama mtu na mgonjwa: mchakato wa tiba
linganishi". Mkutano utafunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayofanyika kwenye
Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Ijumaa asubuhi, tarehe14 Juni 2013.
Askofu
mkuu Zygmunt Zimowski atafungua mkutano huu ili kutoa nafasi kwa mabingwa wa masuala
ya tiba linganishi kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuchangia: weledi, ujuzi na
mang'amuzi yao katika kumhudumia mtoto kama mtu na mgonjwa. Mabingwa hawa wataangalia
magonjwa ya afya ya akili ya mtoto na maendeleo yake; watoto wenye saratani; tiba
kwa watoto wadogo kiakili: madhara na faida zake.
Majadiliano yote haya yanaongozwa
na kanuni maadili "usiumize". Madawa mamboleo: faida na mapungufu yake. Wajumbe pia
watagusia umuhimu wa familia katika kutibu magonjwa ya afya ya akili.Wajumbe pia watapata
fursa ya kujadili masuala haya katika vikundi pamoja na kushirikishana mang'amuzi
yao.
Askofu Nicolas Djomo Lola, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC ataratibu
majadiliano kuhusu tiba ya mtoto mgonjwa na mwelekeo wa jumla. Dr. Angela Anene Okolo
kutoka Nigeria atazungumzia uhusiano uliopo kati ya Daktari na mtoto mgonjwa. Wajumbe
pia watakutana kwa uwakilishi wa Mabara ili kwa pamoja waweze kujadili huduma ya tiba
kwa watoto kama changamoto kwa Kanisa na Jamii: mang'amuzi na ushuhuda kutoka kwa
baadhi ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Duniani.