Waamini wanachangamotishwa kukumbatia sheria ya Mungu
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake siku ya Jumatano tarehe 12 Juni 2013
asubuhi kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae, amewataka waamini kukua na kukomaa
katika sheria ya Mungu inayojikita katika moyo wa mwanadamu, kwa kusikiliza kwa makini
mafundisho ya Yesu, ili kujenga moyo wa ibada na uchaji wa Mungu. Waamini wajifunze
kuwa huru mbele ya Roho Mtakatifu anayewakirimia uhuru mkamilifu zaidi.
Waamini
watambue kwamba, wanaweza kupata uhakika wa usalama wao kwa kukimbilia kwa Roho Mtakatifu
anayewajalia ujasiri na moyo wa kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi katika
mchakato wa kumwilisha Neno la Mungu katika ushuhuda wa maisha.
Baba Mtakatifu
Francisko anasema, katika ulimwengu wa utandawazi kuna mwingiliano mkubwa wa tamaduni
na sheria, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanakumbatia mambo msingi
ya maisha, vinginevyo wanaweza kupoteza dira na mwelekeo wa maisha. Kuna vishawishi
vingi, lakini waamini wawe makini kuisikiliza sauti ya Roho Mtakatifu na sheria ya
Mungu ambayo imeandikwa katika mioyo yao!