Umuhimu wa Familia umebainishwa kwa kina na mapana katika Maandiko Matakatifu. Ni
katika familia mtu hujifunza upendo na uaminifu kwa Mungu na jirani. Hii ni jumuiya
ya kwanza na asili ya binadamu; yenye haki na wajibu wake katika Jamii. Familia inauhusiano
wa pekee katika uhai wa mwanadamu, kwani familia ni chimbuko la uhai na mapendo; mahali
pa kukuza na kudumisha: ukarimu, umoja na mshikamano. Kimsingi familia ni kiini cha
jamii, kumbe wadau mbali mbali wanawajibika kuziwezesha familia ili ziweze kutekeleza
wajibu wake msingi katika Jamii.
Familia ni hekalu ya uhai na chembe hai ya
jamii na ya Kanisa katika ujumla wake. Ni mahali panapofaa kujifunza na kuzoeshwa
utamaduni wa msamaha, amani na upatanisho. Ni mahali ambapo wanafamilia wanaonja na
kuonjeshana: haki, upendo, kazi, wajibu na mamlaka. Familia ni mahali pa kukuza na
kuimarisha maisha ya kikristo kwa njia ya Sala, Sakarementi, Neno la Mungu na matendo
ya huruma. Kimsingi familia kama anavyosema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi
na sita ni mahali pa kuinjilisha na kujiinjilisha ili kushiriki kikamilifu katika
maisha na utume wa Kanisa.
Haya ni kati ya mambo msingi yaliyopelekea Jimbo
Katoliki la Murang'a, nchini Kenya kuanzisha na kuadhimisha Siku ya Familia Kijimbo,
ambayo kwa mwaka huu imefanyika hapo tarehe 9 Juni 2013 na kuongozwa na Askofu mkuu
Charles Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya. Askofu James Wainaina wa Jimbo
Katoliki la Murang'a ndiye aliyekuwa mwenyeji wa maadhimisho haya.
Askofu mkuu
Balvo anawataka waamini kushikamana kwa dhati katika maisha na tunu msingi za kifamilia,
wakitambua kwamba, wao ni Familia ya Mungu inayowajibika, kama walivyobainisha Mababa
wa Sinodi ya kwanza ya Maaskofu wa Afrika. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, wanandoa
walirudia kwa mara nyingine tena ahadi na uaminifu wao katika maisha ya ndoa.
Askofu
James Wainaina anasema, Jimbo limejiwekea mkakati wa ujenzi wa kituo cha mapumziko
kwa ajili ya wanandoa, kinachotarajiwa kuzinduliwa mwezi Agosti, 2013. Hapa patakuwa
ni mahali ambapo, wanandoa watapata nafasi ya kupumzika, kusali na kutafakari kuhusu
maisha na utume wao ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla.
Askofu Charles Daniel
Balvo ameendelea kuwahimiza waamini kusali kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko
katika maisha na utume wake, kwani hii ni dhamana nyeti inayowajibisha sana.