Mwamini anahitaji mwanga wa imani ili aweze kutembea katika hija ya mwanga wa maisha
ya Kikristo, kielelezo cha Sakramenti ya Ubatizo!
Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe kwa Chama cha Vipofu Italia, wakati huu ambapo
kuna kundi la wazee 75 wenye upofu wanaojipumzisha kidogo na kufanya mazoezi kwenye
ufuko wa Bahari mjini Tirrenia.
Baba Mtakatifu anawashukuru wazee hawa kwa
kumkumbuka na kumwombea katika sala zao na kwamba, Yesu alionesha upendeleo wa pekee
kwa watu waliokuwa na upofu, akawaponya na kuwapatia zawadi ya imani. Kila mwamini
anahitaji kupata mwanga wa imani, ili kutembea katika hija ya mwanga wa maisha ya
Kikristo inayopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo.
Baba Mtakatifu
anawaombea wazee hawa ili waweze kuimarika katika imani; wakiwa na mwanga wa uwepo
wa Mungu katika mioyo yao; mwanga ambao ni upendo unaotoa maana ya maisha, unawaangazia
na kuwapatia waamini matumaini na wema kwa ajili ya jirani.
Anawatakia kila
la kheri na baraka kwa kuendelea kuhimiza umuhimu wa kujenga na kudumisha utamaduni
wa kukutana, upendo na mshikamano hasa kwa walemavu, ili nao pale inapowezekana waweze
kushiriki katika maisha ya kijamii.