2013-06-11 07:40:23

Nia za Baba Mtakatifu kwa Mwezi Juni, 2013


Nia za jumla za Baba Mtakatifu kwa Mwezi Juni ni kujenga utamaduni wa waamini kuheshimiana, jambo ambalo linapata chimbuko lake katika majadiliano na hali ya kusikilizana kwa dhati ili kudumisha heshima. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, kumsikiliza jirani yako kwa heshima na taadhima inaweza kuonekana kuwa ni unyonge.

Lakini, hii ndiyo heshima ambayo inafumbatwa katika kitendo hiki cha unyenyekevu hasa ikiwa ni mtu ambaye mnasigana kwa mambo mengi. Majadiliano ni njia muafaka inayoweza kusaidia kukomesha kinzani na migogoro inayoendelea kuibuka siku hadi siku katika Jamii nyingi.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita anabainisha kwamba, katika ulimwengu huu ambamo kuna mwingiliano mkubwa wa watu kuna haja ya kujenga utamaduni wa kuheshimiana; hamu ya kutaka kufahamiana na kuendeleza majadiliano katika hali ya ukweli, unyenyekevu na upendo. Watu watambue kwamba, mbele ya Mwenyezi Mungu ni wadhambi na wanaalikwa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Ni watu wanaohitaji huruma, upatanisho pamoja na kusafisha kumbu kumbu zao katika ngazi ya mtu binafsi na Jumuiya katika ujumla wake.

Hii ndiyo changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa Kichungaji mara baada ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki Mashariki ya Kati, kwani waamini wanachangamotishwa kuwa mashahidi, wanyenyekevu na wenye moyo wa kusamehe, mambo yanayojionesha kwa namna ya pekee kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Itakumbukwa kwamba, Mwezi Juni, Kanisa linafanya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Majadiliano ya kina ni kielelezo cha upendo na mwaliko wa kuuendelea kushirikiana na wengine kwa ajili ya mafao ya wengi.

Majadiliano ya kidini yana umuhimu wa pekee katika ulimwengu wa utandawazi na athari zake, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na mshikamano wa kimataifa. Majadiliano ya kidini ni dhamana na wajibu wa Wakristo na Waamini wa dini nyingine duniani. Kwa Mwezi Juni, Kanisa linaendelea kusali ili kwamba, liweze kusaidia mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa majadiliano.

Nia za Kimissionari za Baba Mtakatifu kwa Mwezi Juni ni Uinjilishaji Mpya, ili pale ambapo watu wamemezwa mno na malimwengu, Jumuiya za Kikristo ziwe ni kikolezo cha Uinjilishaji Mpya. Mwanzoni, nchi nyingi za Ulaya na Marekani zilikuwa mstari wa mbele katika Uinjilishaji wa watu, lakini katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo wanachangamotishwa kwanza kabisa kuwa ni Wamissionari katika nchi na familia zao.

Waamini waliomezwa na malimwengu watambue na kuonja tena umuhimu wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kuna wimbi kubwa la Waamini wanaotoka Kanisani kwa kuona kwamba, kweli na mafundisho ya kiimani hayana tena nafasi katika maisha yao, kiasi cha kudhani kwamba, Mungu hayupo tena!

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto anabainisha kwamba, Uinjilishaji Mpya unakwenda sanjari na toba na wongofu wa ndani. Njia muafaka ya Uinjilishaji Mpya ni kujipatanisha na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani, kwa njia hii waamini wataweza kuona tena ndani mwao ile heshima ya kuwa ni Wana wa Mungu, walioumbwa kwa sura na mfano wake, wakakombolewa kutoka katika dhambi na mauti kwa njia ya Damu Azizi ya Kristo; sasa wanafurahia matunda ya imani ambayo wangependa kuwashirikisha pia jirani zao wale walioko karibu na wale ambao wako mbali.

Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji, kwa kutolea ushuhuda makini kwa Injili ya Kristo na Kanisa lake, hata kwa wale ambao wanaonesha moyo mgumu. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kuwa na ari na mwamko mpya wa maisha ya imani, daima wakijitahidi kuonesha: imani, furaha na matumaini. Ni mwaliko kutoka kwa Yesu kwamba, waamini wote wawe ni wavuvi wa watu kwa njia ya ushuhuda amini wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Uinjilishaji mpya ni njia mpya ya kuzungumza na kutenda katika imani, matumaini na mapendo.








All the contents on this site are copyrighted ©.