2013-06-11 07:52:53

Mapambano dhidi ya biashara haramu ya watoto duniani!


Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 12 Juni inaadhimisha Siku ya Kupambana na Ajira ya Watoto Duniani. Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco kutoka Hispania limezindua kampeni ya kupinga biashara haramu ya watoto ambao wanafanyishwa kazi katika mazingira hatarishi na wakati mwingine kugeuzwa kuwa ni watumwa. Shirika hili kadiri ya taarifa ya FIDES linasema kwamba, kuna zaidi ya watoto 300,000 kutoka Afrika Magharibi wanaopelekwa utumwani kila mwaka.

Baadhi yao wanageuzwa kuwa ni watumishi wa nyumbani, wengine wanapelekwa kufanya kazi katika mashamba makubwa, mashimbo ya madini, kwenye masoko na kwa wasichana wengi wao wanatumbukizwa kwenye soko la ukahaba. Inasikitisha kuona kwamba, kuna nchi kadhaa Barani Afrika zimeweka sahihi itifaki ya kimataifa ya kuwalinda na kuwatetea watoto, lakini bado zinashindwa kuwekeza zaidi katika hatima hii.

Baadhi ya wazazi na walezi kutokana na umaskini na hali ngumu ya maisha wamejikuta wanatumbukia katika biashara haramu ya binadamu, hali inayowanyima watoto hawa fursa ya kusoma na kujiendeleza zaidi. Baadhi ya wazazi wamekuwa wakidanganywa kwa kupatiwa ahadi ya kuwa na maisha bora zaidi pamoja na kupata fedha, lakini matokeo yake ni kuambulia patupu!

Umaskini, tamaa ya fedha na utajiri wa haraka haraka; kinzani na migogoro ya kifamilia; mfumo dume na ukosefu wa usawa miongoni mwa watoto kwani Jamii nyingi za Kiafrika zinawapendelea na kuwekeza kwa watoto wa kiume kuliko ilivyo kwa wasichana. Maadhimisho haya yaikumbushe Jamii umuhimu wa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea watoto dhidi ya watu wenye nia mbaya na watoto hawa!








All the contents on this site are copyrighted ©.