2013-06-11 08:07:04

Majadiliano ya kidini yanapania kukuza mema ya kiroho, maadili, tunu msingi za kijamii na kitamaduni miongoni wa waamini wa dini mbali mbali duniani!


Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia kwa namna ya pekee umuhimu wa Wakristo kuwa na busara na mapendo kwa njia ya majadiliano na ushirikiano na wafuasi wa dini mbali mbali; ni mwaliko wa kutoa ushuhuda wa imani na wa maisha ya Kikristo; kwa kukuza mema ya kiroho, kimaadili na tunu msingi za kijamii na kitamaduni zinazopatikana miongoni mwa wafuasi wa dini mbali mbali duniani. RealAudioMP3

Kwa namna ya pekee, kuna haja kwa Wakristo na Waislam kuendeleza majadiliano ya kidini kama sehemu ya mchakato wa kukuza upatanisho, haki na amani, kwa kufanya kazi kwa njia ya ushirikiano. Hii ni changamoto ya kuondokana na kila aina ya ubaguzi, ukosefu wa uvumilivu na misimamo mikali ya kiimani ambayo wakati mwingine imekuwa ni chanzo cha uvunjifu wa amani na utulivu.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa kichungaji, Africae Munus, Dhamana ya Afrika anawasihi viongozi wa Serikali Barani Afrika kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha uhuru wa kidini: kisheria na kivitendo, ili kila mtu Barani Afrika aweze kuwa na haki ya kuchagua dini anayotaka bila shuruti; akiwa na haki ya kuabudu pamoja na uhuru wa dhamiri.

Kwa kutambua changamoto zote hizi, Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, limeandaa kongamano linalopania kudumisha ushirikiano na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali nchini humo, kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 16 Juni 2013. Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini anatarajiwa kuhudhuria na kuwatembelea viongozi wa dini mbali mbali nchini Uingereza. Lengo la mikutano hii ni kutoa fursa kwa viongozi hawa kuangalia kwa pamoja uwezekano wa kukuza na kuendeleza majadiliano ya kidini, daima wakitafuta mafao ya wengi, haki na amani.

Hii itakuwa ni nafasi kwa viongozi wa kidini nchini Uingereza kusali kwa pamoja hapo tarehe 13 Juni 2013 majira ya jioni kwenye Ukumbi wa Kanisa kuu la Westminster. Wawakilishi wa viongozi wa kidini watatoa sala na maombi yao kwa ajili ya amani kadiri ya mapokeo yao, kama kielelezo cha ushuhuda wa utashi wa amani duniani. Ni sala inayopania kuendeleza mshikamano na udugu ulioanzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, ukaendelezwa na Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kwa kutambua kwamba, majadiliano ya kidini ni jambo msingi kwa ajili ya ujenzi wa amani duniani.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza linasema kwamba, ziara hii ya kichungaji itakayofanywa na Kardinali Jean Louis Tauran itakuwa ni fursa nyingine ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini pamoja na kuimarisha uhusiano uliopo baina ya wafuasi wa dini mbali mbali nchini Uingereza pamoja na kukuza urafiki miongoni mwao!








All the contents on this site are copyrighted ©.