Bado kuna vikwazo vinavyokwamisha mamillioni ya watu duniani kupata huduma bora ya
dawa!
Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za
Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, hivi karibuni wakati akichangia mada kwenye
mkutano wa Baraza la Haki Msingi za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu upatikanaji
wa dawa alisema kwamba, Vatican inaunga mkono mambo msingi yaliyoainishwa kwenye taarifa
iliyotolewa.
Anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya upembuzi
yakinifu na wa kisheria utakaobaini madhara ya kijamii na kisiasa yanayosababisha
mamillioni ya watu kukosa huduma ya dawa ambayo ingesaidia maboresho ya afya ya watu
wengi duniani kutokana na vikwazo mbali mbali vilivyopo kwa sasa. Azimio la Umoja
wa Mataifa linabainisha kwamba, kila mtu anayo haki ya kupata huduma bora ya afya
kwa ajili yake binafsi na familia yake.
Huduma hii ni pamoja na: chakula bora,
malazi safi, nguo, huduma za afya na za kijamii pamoja na kuhakikishiwa usalama wake
wakati wa ukosefu wa fursa za ajira, ugonjwa, ulemavu, hali ya ujane, uzee na mambo
mbali mbali ambayo yako nje ya uwezo wa mwanadamu.
Askofu mkuu Silvano Tomasi
anasikitika kusema kwamba, taarifa hii ina mapungufu kidogo kwani hakuna msisitizo
wa nguvu uliowekwa katika mchakato wa kukidhi mahitaji muhimu ya mtu binafsi na familia,
tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti yanapomfika kadiri
ya mpango na mapenzi ya Mungu. Watu wengi wanashindwa kupata huduma msingi za afya
kutokana na vikwazo vya kisheria, changamoto ya kuweka sheria za haki zinazoongozwa
pia na mshikamano wa kimataifa miongoni mwa watu.
Ujumbe wa Vatican katika
mada hii unapenda kukazia kwa namna ya pekee kuhusu mamillioni ya watu ambayo yanakosa
huduma msingi za afya, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kuangalia uwezekano wa kuanzisha
haki shirikishi inayomhakikishia kila mtu huduma msingi kadiri ya mahitaji yake. Serikali
na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanapotekeleza wajibu wao katika utoaji wa huduma,
kuna haja pia ya kutambua na kuthamini mchango unaotolewa na Mashirika ya kidini katika
mchakato wa kuzuia na kutibu magonjwa ili nao waweze kufaidika na haki zinazotolewa
katika sekta ya afya.
Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anabainisha kwamba,
Kanisa Katoliki ni mdau mkubwa wa utoaji huduma katika sekta ya afya, tangu vijijini
hadi kwenye miji mikubwa duniani. Ni huduma inayotolewa kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii; mahali ambapo hata wakati mwingine, Serikali zinashindwa kutoa
huduma kutokana na sababu mbali mbali. Shirika la Afya Duniani linabainisha kwamba,
kati ya asilimia 30 hadi 70 ya miundombinu ya sekta ya afya Barani Afrika inamilikiwa
na kuendeshwa na Mashirika ya kidini.
Askofu mkuu Tomasi anakiri kwamba, huduma
ya sekta ya afya ni nyeti inahitaji kushughulikiwa kwa umakini mkubwa pamoja na kutambua
mchango unaotolewa na wadau mbali mbali katika sekta ya afya badala ya kujikita zaidi
katika masuala ya sheria, uchumi na siasa.