Askofu mkuu Justin Welby kukutana na kusali pamoja na Papa Francisko, tarehe 14 Juni
2013 mjini Vatican
Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa umoja wa Wakristo linasema, Askofu mkuu Justin
Welby wa Jimbo kuu la Cantebury na Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani duniani, anatarajiwa
kumtembelea Baba Mtakatifu Francisko, mjini Vatican hapo tarehe 14 Juni 2013. Hii
itakuwa ni ziara fupi lakini yenye umuhimu wa pekee kwa viongozi hawa wawili wa Makanisa,
kwa kuwa watakutana na kuzungumza kwa pamoja, tangu wote wawili walipopewa dhamana
ya kuongoza Makanisa yao.
Kwa pamoja wataangalia tena uhusiano wa kiekumene
ulipo kati ya Kanisa Anglikani na Kanisa Katoliki; haki jamii, kanuni maadili, sheria
na kanuni za soko la fedha kimataifa zinazopaswa kuzingatiwa ili kuwaletea watu maendeleo
endelevu. Askofu mkuu Welby tangu aingie kwenye madaraka ametoa kipaumbele cha pekee
katika kukuza na kudumisha upatanisho sanjari na kuhakikisha kwamba, kinzani na migogoro
ndani ya jamii inapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Baba Mtakatifu Francisko kwa
upande wake, anahimiza watu kujenga madaraja ya upendo na mshikamano kati ya watu
wa Mataifa, ili wote waweze kutambuana kama ndugu walioumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu.
Kanisa Anglikani na Kanisa Katoliki yamekuwa na ushirikiano wa karibuni
nchini Uingereza hasa kwa kusimamia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia sanjari
na tunu msingi za kijamii zinazopaswa kudumishwa kwa ajili ya mafao ya wengi, ustawi
na maendeleo ya jamii. Katika ziara hii fupi, Askofu mkuu Welby atafuatana na Askofu
mkuu Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza.
Baba Mtakatifu
Francisko na mgeni wake mara baada ya hotuba, wakati wa mchana kwa pamoja watasali.
Askofu mkuu Welby atapata pia fursa ya kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Petro hadi
chini kabisa ya Kanisa, kama alivyofanya mtangulizi wake, Askofu mkuu mstaafu Rowan
Williams alipotembelea Roma kwa mara ya kwanza.
Askofu mkuu Welby ameomba
pia nafasi ya kusali kwenye kaburi la Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili na atatembelea
Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo, chini ya uongozi wa Kardinali
Kurt Koch.