2013-06-10 08:36:08

Mwilisheni Ibada ya Misa Takatifu katika maisha; Jengeni utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu na Kupokea Sakramenti ya Upatanisho!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani, Jumapili tarehe 9 Juni 2013 limehitimisha Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, lililokuwa linaadhimishwa Jimbo kuu la Colony nchini Ujerumani.

Katika Maadhimisho haya, Baba Mtakatifu amewakilishwa na Kardinali Paul Joseph Cordes, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa linalo ratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum. Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu imekuwa ikifanyika Jimboni humu tangu karne ya kumi na tatu na Siku kuu ya Ekaristi Takatifu imekuwa ikiadhimishwa kwa Ibada na Maandamano makubwa.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Maadhimisho haya anasema kwamba, anapenda kuungana na Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Ujerumani kuonesha umoja wa Kanisa la Kiulimwengu. Mitume walitambua na kuonja njaa ya mwili, iliyowasaidia kujenga na kuimarisha uhusiano wa dhati na Yesu wa Nazareti, wakaimarishwa katika hija ya imani ambayo inawakirimia maisha tele!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wa nyakati hizi kumwendea na kujenga urafiki na Yesu kwa njia ya: kusikiliza kwa makini Maandiko Matakatifu, lakini kwa namna ya pekee katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa ambao ni mwendelezo wa kazi ya ukombozi na maboresho ya maisha ya kiroho kwa njia ya upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujifunza namna ya kumwilisha Ibada ya Misa Takatifu katika maisha yao, kujenga utamaduni wa kumwabudu Yesu katika Sakramenti Kuu pamoja na kupokea Sakramenti ya Upatanisho mara kwa mara. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, mlango wa imani, waamini wamebahatika kuwa ni ndugu zake Yesu Kristo na kwa njia ya Ekaristi Takatifu wanakirimiwa nguvu na ujasiri wa kuendeleza mchakato wa kazi ya Ukombozi.

Baba Mtakatifu Francisko anawachangamotisha waamini kumtolea Kristo ushuhuda wa maisha yao; kwa kutangaza kile walichoona na kusikia kwamba, Yesu anayo maneno ya uzima.Familia ya Mungu inawajibu wa kumpeleka Mungu duniani na dunia kwa Mungu. Kukutana, kujiaminisha na kumtangaza Kristo ni mihimiri mikuu ya imani inayojielekeza zaidi katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa katika Mwaka wa Imani ni kutangaza kwa furaha uwepo endelevu wa Kristo ndani ya Kanisa lake.








All the contents on this site are copyrighted ©.