Askofu Mkude: Umuhimu wa Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti
Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kulisoma,
kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha na vipaumbele vyao. Neno
la Mungu liwaweze waamini kuwa kweli ni vyombo vya haki, amani na upatanisho.
Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika Waraka wake wa kichungaji, Dhamana ya Afrika,
anawahimiza Waamini kushiriki kikamilifu katika utume wa Biblia kwa kuanzia ndani
ya Familia.
Katika sehemu hii ya pili ya Mahojiano kati ya Radio Vatican na
Askofu Telesphor Mkude, Mwenyekiti wa Idara ya Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania anaendelea kukazia umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Familia
za Kikristo, changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu
katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hapa ni mahali ambapo Neno la Mungu
linasomwa, linafafanuliwa, linatafakariwa kwa pamoja na kumwilishwa kwa njia ya matendo.
Askofu
Mkude anasema kwamba, kuna haja ya kuendelea kuimarisha Katekesi kuhusu Fumbo la Ekaristi
Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; kumbu kumbu endelevu ya Sadaka
ya Kristo Msalabani, Ishara ya Umoja na Kifungo cha Upendo, Karamu ya Pasaka na amana
ya uzima wa milele. Waamini wanapompokea Yesu Kristo katika Ekaristi takatifu wanashirikishwa
Umungu wa Kristo kama Yeye mwenyewe alivyoshiriki ubinadamu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho.
Askofu
Telesphor Mkude anasema kwamba, kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, waamini wanapata
ujasiri, nguvu, ari na moyo wa kuweza kumtolea ushuhuda Kristo na Kanisa lake kwa
njia ya imani katika matendo. Anasema Askofu Mkude, huu ni mwaliko kwa waamini kuwa
kweli ni chombo cha: haki, amani, upendo, mshikamano na upatanisho wa kweli.
Kimsingi,
Uelewa wa Neno la Mungu na Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yawachangamotishe
waamini kuwa kweli ni vyombo vya haki, amani na upatanisho kama wanavyokazia Mababa
wa Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika.