Rais Giorgio Napolitano akutana na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 8 Juni 2013 amekutana na kuzungumza na Rais
Giorgio Napolitano wa Italia pamoja na ujumbe wake, ambao baadaye walikutana na kuzungumza
na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu
mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa
mjini Vatican.
Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili wameridhishwa na
uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Italia. Wamejadili kwa kina na mapana hali
ya Italia kwa sasa na mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo ya wananchi
wa Italia. Wamegusia pia masuala ya kimataifa na kwa namna ya pekee, kinzani na migogoro
ya kivita huko Mashariki ya Kati, Kaskazini mwa Afrika pamoja na madhulumu wanayokumbana
nayo Wakristo katika nchi mbali mbali duniani.
Baba Mtakatifu na Rais Napolitano
wameonesha utashi wa kuendelea kushirikiana kwa pamoja katika masuala ya kimataifa
na kwa namna ya pekee, katika harakati za kulinda na kudumisha uhuru wa kidini.