Jubilee ya miaka 100 ya Ukristo Parokia ya Mtakatifu Boniface Aluor, Jimbo kuu la
Kisumu!
Parokia ya Mtakatifu Boniface Aluor, Jimbo kuu la Kisumu, Kenya hivi karibuni imeadhimisha
Jubilee ya miaka 100 tangu ilipoanzishwa kunako tarehe 5 Juni 1913, ikiwa ni Parokia
ya kwanza kabisa kuanzishwa katika eneo la Waluo. Parokia hii imebahatika kupata Parokia
nyingine 19 zilizozaliwa kutoka kwenye Parokia hii mama! Jubilee ya Miaka 100 ya Parokia
ya Mtakatifu Boniface imehudhuriwa na Askofu mkuu Charles Daniel Balvo, Balozi wa
Vatican nchini Kenya.
Katika hotuba yake, Askofu mkuu Zacchaeous Okoth wa Jimbo
kuu la Kisumu, amewashukuru kwa namna ya pekee Wamissionari wa Mill Hill, waliojitoa
bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu na matunda yake yanaonekana.
Askofu mkuu Okoth amewashukuru pia Mapadre Wazalendo waliondeleza kazi ya Uinjilishaji
kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu.
Jubilee hii imepambwa
kwa Majandokasisi wanane kupewa Daraja la Ushemasi, kielelezo cha huduma ndani ya
Kanisa. Kigango cha Mtakatifu Pantalion kimepandishwa hadhi na kuwa ni Parokia Mpya
na Padre Paul Oduor ameteuliwa kuwa ni Paroko wake wa kwanza.
Askofu mkuu Balvo
katika mahubiri yake, amewataka Mashemasi wapya kujitosa kimaso maso kutangaza Injili
ya Kristo hadi miisho ya dunia. Watambue kwamba, kwa Daraja la Ushemasi, wanakuwa
ni sehemu ya wajenzi wa Ufalme wa Mungu uliojionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya
Sadaka ya Kristo Msalabani. Kama Mashemasi wanaitwa na kutumwa kumhudumia Kristo aliyeteswa,
akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 100 ya Parokia
ya Mtakatifu Boniface Aluor sanjari na Mwaka wa Imani, yawe ni kikolezo cha imani
tendaji katika maisha na vipaumbele vya waamini wa Jimbo kuu la Kisumu, Kenya.