2013-06-08 08:00:53

Askofu Mkude anachambua kwa kina na mapana Ukuu na Utukufu wa familia


Familia katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo zinakabiliwa na changamoto, matatizo na fursa mbali mbali katika maisha na utume wake kwa Kanisa na Jamii kwa ujumla. Askofu Telesphor Mkude, Mwenyekiti wa Idara ya Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anayefafanua umuhimu wa Familia katika Jamii kadiri ya Mpango wa Mungu. RealAudioMP3

Mwanadamu ni sehemu ya mpango wa kazi ya uumbaji, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; hali inayoonesha utukufu na ukuu wa mwanadamu, changamoto kwa waamini kuendeleza ndani mwao ile neema ya utakaso waliyoipokea wakati wa Sakramenti ya Ubatizo, kwani dhambi ya asili iliharibu ule utukufu ambao Mwenyezi Mungu alikua amemkirimia mwanadamu wakati alipokuwa anamuumba.

Askofu Mkude anasema kwamba, lengo la Familia ni kusaidiana, kuhudumiana na kukamilishana ili kuufikia utakatifu wa maisha, ambalo ndilo lengo kuu. Wanandoa wamekabidhiwa dhamana ya kushiriki na kuendeleza ile kazi ya uumbaji, kumbe wanapaswa kupendana na kuheshimiana katika taabu na raha; magonjwa na afya. Hii ni dhamana nyeti sana kwa maisha ya mwanadamu kwa sasa na kwa ajili ya kizazi kijacho.

Baba na Mama wanalo jukumu la kuanzisha Familia na kwamba, watoto ni zawadi na m atunda ya upendo kati ya mwanaume na mwanamke kadiri ya mpango wa Mungu na wala si vinginevyo! Ikumbukwe kwamba, kila mtoto ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukumbatia na kuenzi Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni na sera za kifo zinazopigiwa debe sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu Mkude anabainisha kwamba, Familia ni chimbuko na asili ya kila binadamu: inapaswa kutambuliwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa kwa Mwaka 2011 iliyoadhimishwa Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia, alikazia umuhimu wa Familia kukuza na kuimarisha umoja na mshikamano! Taasisi, Serikali na watunga sheria na sera wazisaidie Familia kutekeleza wajibu na dhamana yake katika Jamii na kamwe wasiwe ni vikwazo.

Elimu na malezi kwa watoto ni dhamana na jukumu la wazazi. Kutokana na changamoto na matatizo mbali mbali yanayoendelea kujitokeza, Familia inapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuhifadhiwa kwa nguvu zote. Familia ipewe fursa ya kufanya kazi na kupata ujira halali utakaoiwezesha kupata mahitaji yake msingi na kuishi katika hali ya kiutu. Familia ziwezeshwe kutekeleza dhamana ya kuboresha ulimwengu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kutambua na kuthamini uwepo wa Mungu anayezitegemeza Familia.

Familia ijenge utamaduni wa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa; lakini zaidi kwa kuhudhuria katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ili: kumshukuru, kumtukuza, kumwabudu na kumwomba Mwenyezi Mungu. Jumapili ambayo kimsingi ni "Siku ya Bwana" "Dies Domini" ni Siku ya Sherehe kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa yote aliyowakrimia katika kipindi cha juma zima.

Hii ni changamoto kwa Waamini kukusanyika Makanisani ili kujiunga na jirani zao kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Wanapasa nafasi ya kushiriki Meza ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu, changamoto ya kuwa ni Ekaristi kwa jirani zao.







All the contents on this site are copyrighted ©.