2013-06-07 07:57:26

Simameni kidete kutangaza Injili ya Uhai Duniani!


Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya anasema kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, hapo tarehe 15 hadi tarehe 16 Juni 2013 yatakuwa na sura ya pekee, pale ambapo waamini kutoka pande mbali mbali za dunia watakapokusanyika kusali, kutafakari na kushuhudia pamoja na Baba Mtakatifu Francisko umuhimu wa zawadi ya maisha ambayo mwanadamu amekabidhiwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. RealAudioMP3

Hii ni zawadi ambayo inapaswa kulindwa na kuheshimiwa, tangu pale mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi na mpango wa Mungu. Ni zawadi ya maisha inayojionesha miongoni mwa wazee na wagonjwa walioko kufani, wanaonyemelewa na utamaduni wa kifo kutokana na baadhi ya watu wachache ndani ya Jamii kutaka kukumbatia sera za kifo laini na utaoaji mimba, mambo ya kutisha lakini baadhi ya watu wanaanza kuyaona kuwa ni ya kawaida.

Askofu mkuu Fisichella anasema kwamba, hii itakuwa ni fursa maalum ya kuendelea kuwatia shime, wale wote wanaosimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha, huku wakijitahidi kufuata nyayo za Kristo mchungaji mwema, kwa kuwamegea watu utajiri unaobubujika kutoka katika Injili ya Kristo, kwani Kristo mwenyewe anasema, “Mimi nalikuja ili wawe na uzima, kasha wawe nao tele”. Hiki ndicho kiini cha Ujumbe uliomo kwenye Waraka wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, Evangelium Vitae, Injili ya Uhai.

Askofu mkuu Fischella anasema, watu wengi wameonesha nia ya kushiriki katika tukio hili la kihistoria wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani, ili umati wa waamini na watu wenye mapenzi mema utakaokuwa umekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, uweze kupiga kelele ya kutetea Injili ya Uhai hadi miisho ya dunia.

Kwa siku mbili, Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjili Mpya litaendesha semina elekezi kuhusu yaliyomo kwenye Waraka wa Kichungaji wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, Injili ya Uhai. Mama Kanisa anapenda kuhakikisha kwamba, Injili ya Uhai inaendelea kupewa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya.

Tarehe 15 Juni 2013, Warsha kwa ajili ya wazungumzaji wa Lugha ya Kiingereza itafunguliwa kwenye Chuo Kikuu cha Urbaniana. Kardinali Raymond Leo Burke atatoa hotuba elekezi. Askofu mkuu Joseph Augustine di Noa ataongoza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwenye Kanisa la Santo Spirito in Sassia, lililoko karibu na Vatican na baadaye yatafuatia Maandamano ya waamini wakiwa wamebeba mishumaa kuelekea kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro, kwa ajili ya sala na kesha.








All the contents on this site are copyrighted ©.