2013-06-07 15:10:34

Siku ya Dunia ya kuombea Utakaso wa Mapadre


Tarehe 7 Juni Mama Kanisa huadhimisha Siku Kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambayo pia ni Siku ya Kimataifa kwa ajili ya kuombea Utakatifu wa Mapadre.
Askofu Mkuu Morga Iruzubieta, Katibu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makreli, akilizugumzia adhimisho hili amesema, katika muono wa Mwaka wa Imani, inakuwa ni mwaliko wa kutafakari - katika mwanga wa imani yenyewe - kwa nini Padre Katoliki ni muhimu sana kwa Kanisa na kwa watu wote. Na uwepo wa utume wake, hauzeeki au kuwa wa mpito na wala si wa kupuuzwa kwa sababu, Padre daima huwa na ujumbe muhimu wa kuwasilisha kwa watu, hasa kwa jamii ya kisasa, iliyotawaliwa na ukana Mungu, kupenda mali na itikadi za mamlaka tawala mbalimbali .
Askofu Mkuu Morga, ameendelea kueleza kwa nini Padre Katoliki ni muhimu sana kwa dunia ya leo, kuwa yeye ni mjumbe na mwakilishi wa jamii na hasa kumuiya za watu maskini na wanyonge ambao sauti zao haziwezi kusikilizwa na jamii,katika kutetea haki na amani yao. Katika hali hizo Padre anakuwa wakili wa jumuiya hizo kwa mashirika na serikali na kwa ajili ya manufaa ya wote. Na zaidi ya yote, Padre anao umuhimu wa kipekee kwa sababu, humwongoza mtu kiroho na kimwili, kutembea katika nji ya maisha ya uzima wa milele.
Amefafanua binadamu katika asili ya umoja wa roho na mwili, ndani mwake ana uwezo wa kupambanua mema na mabaya, ndani mwake mna sauti ya wokovu inayomwita, kuifuta njia inayofaa , lakini kwa uhuru kamili aliopewa na Muumba wake , kama ilivyoandikwa katika waraka wa Kanisa katika nyakati hizi (Gaudium et Spes, 14).
Hivyo Upadre ni dhamana ya Mungu, ambayo huitoa kwa yule aitwaye katika kazi ya kuhudumia watu kwa yale yanayotakiwa kufanyika katika hija ya maisha hapa duniani , jinsi ya kutembea, jinsi ya kupumua hewa safi ya kiroho na jinsi ya kuishi hadi kuufikia uzima wa milele. Katika jina la Yesu Kristo, Padre ni mtumishi wa watu katika hali zote za maisha.
Mapadre kama watumishi wa wokovu wa milele, kwa wanao isikia sauti ya Mungu na kusadiki, katika mwanga wa ufunuo, huzamishwa katika kina cha nafsi ya binadamu, na bila mipaka, huchambua, kutathmini na kutoa ufumbuzi katika uzushi wa kidunia na furaha zake za mpito zinazokuwa kikwazo kwa mtu kuupata uzima wa milele.
Askofu Mkuu Morga amemalizia ujumbe wake kwamba, Padre wa kweli wa Kristo, kamwe hawi mtu wa zamani katika kuwaongoza watu wa kila umri na hali. Kwa njia na mbinu mbalimbali humsaidia mtu kuizamisha nafsi yake mwenyewe katika vilindi vya kuigundua sura ya Mungu, na uwezo wa kujua na kumpenda Muumba wake, kama mwana wake katika Kristo. Ni katika Upendo tu huu , mtu huweza kugeuka na kubadilisha maisha yake, akiondokana na giza na mashaka katika imani. Hupata jibu la kweli linalo mwinua katika ubinadamu wake , jibu lenye kumwondoa katika itikadi mbalimbali za kupenda mambo ya dunia na mali, vyenye kumfanya mnyonge na kama vile hana maana.








All the contents on this site are copyrighted ©.