Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza anatarajiwa kushiriki katika mjadala kuhusu
Amri 10 za Mungu, tukio ambalo limeandaliwa na Chama cha Kitume cha Uamsho wa Roho
Mtakatifu kwa kutuma ujumbe kwa njia ya video, Jumamosi, tarehe 8 Juni 2013. Tukio
hili linafanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Milani, Kaskazini mwa
Italia. Wakati huu, washiriki wa kongamano hili wanajadili kuhusu Amri ya Tatu: Shika
kitakatifu siku ya Mungu.
Yote haya ni matukio yanayokwenda sanjari na changamoto
ya Uinjilishaji Mpya iliyotolewa na Mama Kanisa wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani na yatafanyika sehemu mbali mbali za Italia. Itakumbukwa kwamba, kwa mara
ya kwanza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako Mwezi Septemba 2012, alizindua
Maadhimisho haya mjini Roma, kwa kujadili Amri ya Kwanza "Ndimi Bwana Mungu wako,
usiabudu Miungu wengine".
Baadaye tarehe 15 Septemba 2012 maadhimisho haya
yalifanyika mjini Verona kwa kutafakari Amri ya pili "Usilitaje bure jina la Mungu
wako". Mjini Napoli, wao walitafakari Amri ya Nne "Waheshimu Baba na Mama Upate Miaka
mingi na heri duniani". Ni kongamano ambalo linawashirikisha watu kutoka medani mbali
mbali za maisha.