2013-06-07 07:44:45

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Siku ya kuombea utakatifu wa Mapadre


Wapendwa Taifa la Mungu, nawatakieni amani na salama katika mapendo ya Moyo Mtakatifu wa Kristo. Leo Mama Kanisa anasherehekea Sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Moyo uliochomwa mkuki pale msalabani mara ikatoka damu na maji, kielelezo cha Sakramenti za Kanisa. RealAudioMP3
Kumbe, Mama Kanisa anasherehekea chemchemi ya neema za Mungu, anasherehekea zawadi ya upendo katika maisha yake. Sherehe hii ni kati ya sherehe za Bwana kadiri ya mpango wa kiliturujia ambayo huja kila Ijumaa ya pili baada ya Sherehe ya Pentekoste.
Mara moja tunaposikia neno Moyo Mtakatifu wa Yesu, tunapaswa kukumbuka maneno ya Mtakatifu Yohane, asemaye “tazama jinsi Mungu alivyoupenda ulimwengu”. Bila shaka Mtakatifu Yohane anataka tutambue kuwa mapendo ya Mungu kwa wanadamu wote na kwa vizazi vyote hayana kikomo na wala ubaguzi. Kanisa likitafakari zawadi hiyo kubwa ya mapendo ya Mungu kwa wanadamu wote, haliachi kutumia zawadi hiyo kusogeza karibu neema za Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa waamini wake maklero kwa walei, ndiyo kusema leo pia ni sikukuu ya kutakatifuzwa kwa mapadre.
Wapendwa taifa takatifu, tukiwa na nia njema tumfuase Bwana tukitafakari Neno lake ambalo Mama Kanisa ametuwekea leo hii ili kwalo tutambue mapendo ya Mungu yatokayo katika Moyo wake. Katika somo la kwanza Mungu anaongea na Waisraeli kwa njia ya Nabii Ezekieli.
Anatangaza mapendo yake kwao akiwahakikishia ukombozi toka utumwa wa Babeli na kwingineko walikokuwa wametawanyikia kwa sababu ya nchi yao kutekwa. Katika kutawanyika basi wengine wamepata majeraha kama kondoo waliojeruhiwa na zaidi majeraha ya kiroho. Mwenyezi Mungu ambaye anajitokeza kama mchungaji wa kondoo katika mafuriko ya upendo toka Moyo wake anatangaza usalama na amani ya kwamba atawalaza katika malisho ya majani mabichi na katika nchi inayokaliwa na watu, kwa kifupi atawarudisha nyumbani katika nchi yao.
Haya kwa hakika ndiyo hasa makusudio makamilifu yaliyo katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, yaani kuleta uhuru kwa watu na kutangaza ukombozi wa milele. Nabii Ezekieli anasisitiza kwamba Mungu mwenyewe atachukua jukumu la kulinda na kuchunga kondoo wake, jukumu litokalo katika moyo wake. Tena anarudia mara tatu jambo hilo akitaka kuonesha ukamilifu wa shughuli yenyewe.
Pamoja na shida yao iliyowafanya waende utumwani Mungu hatangazi visasi wala adhabu, kumbe sisi tu watu wake na kondoo wa malisho yake hata katika kumwacha yeye na kuwafuata wafalme wengine wa dunia.
Mpendwa, hicho anachokitangaza Nabii Ezekieli katika Agano la Kale kinakamilika katika Agano Jipya ambapo tunamwaona Bwana wetu Yesu Kristu akitangaza kwa upendo mkamilifu kuwa yeye ni Mchungaji Mwema ambaye hutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake (Yn 10:11). Haya ndiyo mapendo ambayo Moyo Mtakatifu wa Yetu wataka kutupa na kutufundisha na zaidi kwa vizazi vyote.
Hata hivyo basi, tunaalikwa kuitika mapendo ya Mungu kwa kuisikia sauti ya mchungaji mwema na hapo ndipo kuna uhai kama Mzaburi asemavyo "sheria ya Mwenyezi Mungu ni kamilifu, humpa mtu uhai mpya (Zab. 19:7). Huo ndio mwitiko wa mkristo na awaye yote katika kupokea mapendo yatokayo katika Moyo Mtakatifu wa Yesu na hata ikibidi kuimba kila siku Bwana ndiye mchungaji wangu sitapungukiwa na kitu (Zab. 23:1).
Katika somo la kwanza tumepata kusikia na kutafakari jinsi Moyo wa Mungu unavyojari na kutenda yote kwa ajili ya ustawi wetu, kumbe tuna hakika ya usalama na amani. Katika hilo Mtakatifu Paulo anapowaandikia Warumi anakazia pendo la Mungu ambalo limemiminwa katika mioyo yetu kwa njia ya Roho Mtakatifu, Mungu mfariji na mwalimu wa mapendo. Pendo lililomiminwa kwetu linatoka katika kisima cha mapendo yaani Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Ahadi ya Bwana ya kumpeleka Roho Mtakatifu inaambatana ndani mwake na mapendo makamilifu ya Mungu kwa vizazi vyote. Mt Paulo anasema wakati ule tulipokuwa hatuna nguvu basi Kristo alikufa kwa ajili yetu ili tujazwe na pendo la wokovu wa milele. Tena Mtakatifu Paulo akisisitiza upendo wa Mungu kwetu anakuja na tendo la mtu kufa kwa ajili ya mtu mwingine kuwa ni tendo la kuonesha upendo upeo.
Kristo amekufa na kufufuka kwa ajili ya ulimwengu mzima, ni jambo la ajabu lakini ndicho kielelezo cha juu cha mapendo ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa mwanadamu. Mungu kwa jinsi hiyo haadhibu bali hutoa zawadi kwa wote katika uhuru wake kwa maana hakuna anayeweza kusema mimi nastahili.
Tusomapo Injili ya Matayo tunaona Matayo anatupa kielelezo cha mapendo ya Mungu kwa kutoa mwaliko akisema: njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha" Mt 11:28. Mwaliko ni kupumzika katika Bwana. Leo hii tunatafakari somo toka Injili ya Mt. Luka 15:3-7 ambapo tunakutana na mwendelezo wa fundisho la Mungu kwa njia ya Nabii Ezekieli juu ya kondoo.
Nabii Ezekieli tuliona Mungu akiwatafuta kondoo walio katika mahangaiko na akihaidi kuwalaza katika majani ya malisho mabishi na pia kuwarudisha nyumbani. Bwana anatoa mfano wa mchungaji atafutaye kondoo mmoja aliyepotelea machungani kwa kuwaacha 99. Anataka kufundisha kuwa hakuna atakayeachwa katika ufalme wake. Kwa hakika kiuchumi hakuna mantiki sahihi, yaani mmoja kuacha mali ya thamani kubwa akifuatilia mali ya thamani ndogo! Lakini hii ndiyo mantiki ya Kimungu, ni mantiki ya upendo mkamilifu.
Mpendwa mwana wa Mungu katika jumuiya ya Kiyahudi kuna mahangaiko na mbegu ya dhambi imeshamiri na hivi baadhi ya Mafarisayo na Waandishi wanaamini kuwa Mungu hawezi kuwasamehe na hivi linalobaki ni kupatilizwa. Hawa wanafikiri hivyo kwa sababu haki kwao ni kulipa kadiri ya matendo au kadiri ya kazi iliyofanyika. Hivi leo hata sisi twafikiri namna hii wakati fulani tunapozama katika ubinafsi wetu.
Mpendwa mwana wa Mungu, toka somo la Injili, huruma ya Mungu yazidi upeo wa kifarisayo na hata upeo wetu, ni huruma ambayo haiangalii gharama na mipango ya kiuchumi bali huangalia thamani ya kiumbe ikikumbuka “Mungu akaona kila kitu alichokifanya kuwa ni chema kabisa, ikawa jioni, ikawa asubuhi siku ya sita” (Mw. 1:31). Kwa namna hiyo basi matendo yake hayawezi kupingana na makusudio yake tangu mwanzo alipoumba ulimwengu.
Kristo mchungaji mwema anatenda kazi ileile ya Baba yake pasipo kupindisha hata nukta ya kusudio kwa sababu yeye na Baba ni wamoja. Basi katika hilo tunaomwona daima Mwinjil Mt. 9:12 akinukuu maneno ya Bwana akisema mwenye afya hamhitaji tabibu bali aliye mgonjwa na Mwinjili Luka 4:18 akinukuu maneno ya Nabii Isaya ambayo yaliratibishwa na Bwana anasema Roho wa Bwana amenituma kuwahubiria maskini habari njema. Haya yote tunayoyasikia ni matokeo ya mapendo ya Moyo Mtukufu wa Bwana.
Mpendwa msikilizaji, sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni sikukuu ya Mapendo ya Mungu kwa Wanadamu wote, ni Sikukuu ambayo Mama Kanisa ataka kukazia umisionari wa Mapendo hapa duniani ambao unaanzia katika Moyo wa Bwana na polepole kuenea katika Kanisa na familia zetu. Kama ambavyo Kristu anatoa Moyo wake uchomwe mkuki na baadaye zinatoka zawadi za kiroho basi nasi katika maisha yetu tuchomwe na moto huo wa mapendo na kuwa harufu na manukato mazuri kwa ajili ya kuponya majeraha yatokanayo na migawanyiko na machafuko ya kivita katika ulimwengu wetu. Moyo Mtakatifu wa Yesu utukumbushe amani na salama katika familia zetu na Parokia zetu.
Mpendwa msikilizaji leo pia tunawakumbuka Mapadre wetu kama wagawaji wa mafumbo matakatifu ya kuwatakatifuza wengine basi nao wanahitaji zawadi ya sala. Mwanzoni wa Utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Papa Francisko aliwaomba waamini wote wamwombee, basi nami nawaomba waamini wote tuombeeni sisi mapadre wenu ili daima kama Moyo wa Bwana ulivyochomwa mkuki na kutoa zawadi za mbinguni basi nasi tuchomwe mioyo yetu na tuwe madaraja ya waamini kufika kwa Bwana.
Mpendwa ninakukumbusheni kuwa ahadi za Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kwa vizazi vyote na kwa kifupi wote watakao sali daima katika mapendo ya Moyo huo watakirimiwa zawadi zote za kiroho na zaidi sana uzima wa milele. Tunawatakieni heri na Baraka tele zitokazo katika Moyo Mtakatifu wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C. PP. S.








All the contents on this site are copyrighted ©.