2013-06-06 15:19:56

Papa Francis asema kumlilia Mungu wakati wa shida si dhambi


Kumlalamikia Mungu wakati wa mateso si dhambi ila ni sala inayotoka ndani ya Moyo wa muumini kwa Bwana wake. . Ni tafakari ya Papa Fransisko wakati wa Ibada ya Misa, Jumatano asubuhi, katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta la Vatican. Ibada iliyohudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa Shirika la Kipapa kwa ajili ya Ibada na Nidhamu katika Sakramenti , pia walikuwepo wafanyakazi wa Idara ya Maktaba ya Kitume ya Vatican. Papa alisaidiana na Kardinali Antonio CaƱizares Llovera; Askofu Mkuu Joseph DiNoia,na Monsignor Cesare Pasini.
Homilia ya Papa ililenga zaidi katika ujumbe wa somo la kwanza, maana ya maisha ya kuteseka ya Tobiti na Sara. Tobit, aliye pofuka licha ya kuwa mtu mwema, aliyetenda mengi mema na hata kuhatarisha maisha yake. Na Sara, mwanamke aliyeposwa na wanaume saba , na wote kufariki usiku wa kabla ya harusi.
Papa anasema,watu hao, kila mmoja alimlalamikia Bwana uchungu mkali toka moyoni mwake. Waliomba kwa Mungu, hata kifo kiwafike, na walijaribu kila njia ya kujiondoa katika matatizo yao. Walimlalmikia Mungu lakini hawakukufuru. Na hivyo, hili linatuonyesha kwamba, kuomboleza mbele ya Mungu si dhambi.
Papa alieleza na kutoa mfano mwingine wa mama mmoja aliyekwenda kwa Padre, kumlalamikia Mungu kwa Mateso anayoyapata.Na Padre alimwambia mwanamke huyo, Mama malalamiko ni sehemu ya sala zako hivyo endelea nayo, Bwana anasikia, malalamiko yako.
Papa aliendelea kutaja mifano mingine mingi mbalimbali ya watu walioteseka mfano wa Ayubu, aliyesema, na ilaaniwe siku niliyozaliwa, na Yeremia, pia alimlalamikia Mungu akisema na ilaaniwe siku niliyozaliwa. Siku hiyo mama aliponizaa, isiwe siku ya Baraka.
Papa anasema, kwa ubinadamu wao, waliyalalamikia mateso yao kwa Bwana, lakiini hawakukufuru.

Baba Mtakatifu pia aliyatazama malalamiko ya watu wa kale katika mateso, akilinganisha na wakati wetu, kwa mfano watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi mitaani, wale wenye utapiamlo mkali, wakimbizi na wagonjwa mahututi n.k.
Na alionya dhidi ya kufikiria mateso ya wengine kijuu juu bila ya kuwa na bidii za kufanya linalo wezekana kuwasidia katika mateso yao. Alikemea tabia ya kuzungumzia hali ngumu kwa namna za kitaalumbila ya kutazama utu na heshima yao kama binadamu. Alisema, hata katika kanisa kuna watu wengi katika hali hii..

Papa amehimiza katika hali hizo , Mkrisu anapaswa kufanya kama Yesu alivyosema, salini, kwa ajili yao. Sala hizo ni lazima zitoke ndani ya moyo, ni lazima iwe sababu ya kukosa utulivu wa kiroho kwa ajili ya mateso binafsi, na kwa ajili ya ndugu zetu walio katika mateso na kifo. Kumwomba Bwana kutoka kina cha moyo na si kulalama tu kijuujuu. Papa alimalizia kwa kutoa wito kwa waamini wote, kuomba kwa uaminifu kwa ajili ya wale ambao wanaishi hali ya mateso makubwa kama vile Yesu juu ya msalabani ,wanalia Baba, Baba, kwa nini umeniacha? Tusali ili maombi yetu yafike mbinguni na iwe chanzo cha matumaini kwa sisi wote.








All the contents on this site are copyrighted ©.