2013-06-06 10:19:50

Kauli mbiu ya Siku ya Mazingira duniani kwa Mwaka 2013: Fikiri kwanza, kula na hifadhi mazingira!


Kila mwaka ifikapo tarehe 5 Juni, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Mazingia Duniani kutokana na Azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa la Mwaka 1972 ikiwa ni kielelezo cha ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira uliofanyika huko Stockholm, nchini Uswiss.

Aidha, Azimio la kuunda Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Mazingira Duniani, yaani UNEP, pia lilipitishwa siku hiyo. UNEP ni chombo pekee cha Umoja wa Mataifa chenye makao makuu yake Barani Afrika, huko Nairobi, Kenya.

Lengo kubwa katika kuadhimisha siku hii Kimataifa na kitaifa ni kuweka msisitizo katika masuala ya mazingira na kuwapa uwezo wananchi ili wawe mawakala wazuri wa maendeleo endelevu. Pili ni kutoa nafasi ya kutafakari kuhusu hali na umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira, kuelimishana na kukuza ari ya wananchi kushiriki katika shughuli za hifadhi na usimamizi wa mazingira yao.

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kimataifa yatafanyikia nchini Mongolia, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Fikiri, Kula: Hifadhi Mazingira” au kwa lugha ya Kiingereza ”Think – Eat – Save”. Ujumbe huu unawakumbusha watu na kuwahimiza kutekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kuhakikisha kuwa shughuli za uzalishaji mali na utoaji wa huduma zinakuwa rafiki wa mazingira na kamwe zisiwe chanzo cha uharibifu wake.

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira kwa Mwaka huu yamelenga kuwahamasisha watu kutumia vizuri chakula kilichopo sanjari na utunzaji bora wa mazingira. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa linabainisha kwamba, kuna kiasi kikubwa cha chakula kinachotupwa tangu pale kinapozalishwa hadi hatua ya mwisho ya kumfikia mlaji.

Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga utamaduni wa kuwa na matumizi bora ya chakula kwani inakadiriwa kwamba, ifikapo mwaka 2050 idadi ya watu duniani itakuwa imefikia walau billioni tisa. Matumizi bora ya chakula ni jambo linalopaswa kuangaliwa: kiuchumi, kijamii na kimaadili anasema Bwana Achim Steiner, Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia mazingira duniani.








All the contents on this site are copyrighted ©.