2013-06-06 11:24:28

Kanisa Barani Afrika halina budi kuanza mchakato wa kulitegemeza Kanisa


Kanisa Barani Afrika linakabiliwa na changamoto ya kulitegemeza Kanisa ili liweze kutekeleza dhamana na wajibu wake wa Uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema rasilimali watu, vitu na fedha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia, kwa kutambua kwamba, ujenzi wa Kanisa la Afrika unawategemea zaidi Waafrika wenyewe.

Umefika wakati kwa waamini Barani Afrika kujenga moyo na ari ya kujiamini katika majukumu yao ndani ya Kanisa na kuondokana na kasumba ya kutegemea misaada kutoka nje ya Bara la Afrika kwani hali imebadilika na wanapaswa kusoma alama za nyakati.

Ni changamoto na mwaliko uliotolewa hivi karibuni na Askofu Martin Kivuva wa Jimbo Katoliki la Machakos, Kenya wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Kisasa la Parokia ya Mitaboni, Jimboni humo. Kiasi cha shilingi za Kenya millioni 1.6 zilikusanywa kutoka kwa waamini na wananchi wenye mapenzi mema walioshiriki katika harambee hii.

Askofu Kivuva anasema kwamba, ikiwa kama waamini watamegemea Mwenyezi Mungu na kumwendea kwa kwa sala na unyenyekevu anaweza kutenda miujiza, kiasi cha kuwashangaza. Ameipongeza Familia ya Mungu Parokiani hapo kwa kujitoa kimasomaso kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa. Kanisa nchini Kenya litaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu na kwamba, Serikali isaidie kuchangia upatikanaji wa waalim ili Kenya iweze kucharuka kwa maendeleo katika sekta ya elimu.

Askofu Kivuva amefanikiwa kuchangisha kiasi cha shilingi millioni 2.3 kwa ajili ya Ujenzi wa Seminari ndogo ya Papa Paulo VI, iliyoko Katoloni, Jimboni Machakos. Jumuiya ndogo ndogo zimehusishwa kikamilifu katika mchakato wa kulitegemeza Kanisa kuanzia katika ngazi mbali mbali hadi kufikia kilele chake kwa Siku ya Tegemeza Jimbo, inayowakusanya waamini wa Parokia na Taasisi zote za Kanisa husika.







All the contents on this site are copyrighted ©.