Ekaristi Takatifu ni kifungo cha upendo, umoja, amani na mshikamano!
Maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu kwa Mwaka 2013 yamekuwa na uzito wa pekee
kutokana na Mama Kanisa kuendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani, changamoto kwa Waamini
kumshuhudia Kristo katika maisha na vipaumbele vyao. Ni tukio ambalo limewaunganisha
Wakatoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia chini ya Baba Mtakatifu Francisko kuabudu
Ekaristi Takatifu kwa wakati mmoja.
Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu
ni kielelezo cha hija ya maisha ya Wakristo, wanaoitwa na kukusanywa na Kristo kwa
ajili ya kujenga na kuliimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ni mwaliko
wa kushiriki na kujenga: misingi ya haki, amani na upatanisho; umoja na mshikamano
mambo yanayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hii ni meza ya
Neno la Mungu na chakula cha maisha ya uzima wa milele, changamoto ya kuhakikisha
kwamba, waamini wanaishi katika neema ya utakaso na kifungo cha upendo.
Ni
changamoto ambayo imetolewa na Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma katika
Maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu, iliyoshuhudia watoto 917 kutoka Dekania
ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba wakipokea Komunio ya kwanza kwenye Kituo cha Hija cha
Mbwanga, Jimbo Katoliki Dodoma.
Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa
kuendelea kuwa ni mashahidi wa amani, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wanaowazunguka.
Askofu Nyaisonga amewataka watanzania kwa ujumla kudumisha misingi ya amani, upendo,
umoja na mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote.
Wanandoa wadumishe tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; watekeleze wajibu na
dhamana ya malezi na elimu kwa watoto wao.
Waamini wa Dekania ya Mtakatifu
Paulo wa Msalaba Jimbo Katoliki Dodoma walitoka kwa maandamano na nyimbo, kuelekea
kwenye Kituo cha Hija cha Mbwanga, hapo wakakusanyika kuadhimisha Fumbo la Ekaristi
Takatifu. Hili ni tukio ambalo wanasema wachunguzi wa mambo limeacha guzmo la pekee
mjini Dodoma.