Askofu mkuu Ruzoka: Tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi ni hatari kwa misingi
ya taifa!
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Rasimu ya Katiba yake inabainisha misingi mikuu
ya Taifa kuwa ni: uhuru, haki, udugu, usawa, umoja amani na mshikamano. Inapania kuenzi
na kuzingatia Tunu za Taifa zifuatazo: utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji,
na lugha ya Taifa. Watu wenye mapenzi mema na wapenda amani duniani wanaendelea kujiuliza
nini ni chimbuko la watu nchini Tanzania kuanza kujichukulia sheria mikononi mwao,
hali ambayo kwa sasa inaanza kuonekana kwamba inajenga mazoea.
Askofu mkuu
Paul Ruzoka, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
anasema, tabia hii inaleta madhara makubwa kwa wahusika wenyewe, lakini zaidi inadumaza
maendeleo na hivyo kusababisha maafa na uharibifu mkubwa wa maisha na mali za watu.
Ni
vitendo vinavyovuruga misingi ya haki, amani, upendo na utulivu miongoni mwa watanzani,
tunu ambazo Tanzania imekuwa ikijivunia tangu ilipojipatia uhuru wake takribani miaka
51 iliyopita. Kuna haja kwa wadau mbali mbali kuchunguza kwa makini ili kubaini chanzo
cha vurugu hizi.
Hata hivyo Askofu mkuu Ruzoka anabainisha kwamba, kuna haja
ya kujenga na kudumisha misingi ya utawala bora; utawala unaozingatia utu na heshima
ya kila mtu pamoja na sheria za nchi.
Wadau wanaohusika kusimamia na kutekeleza
sheria na kanuni za utawala bora wanapaswa kutekeleza wajibu wao barabara sanjari
na kudhibiti magenge ya watu wanaochochea fujo na vurugu za kijamii, ili mambo haya
yasigeuke kuwa ni sehemu ya utamaduni wa watanzania. Yote haya yatekelezwe kadiri
ya sheria na taratibu za nchi.