Wanafunzi kufundwa somo la sayansi na hisabati na walimu kutoka Japan!
Tanzania imeiomba Japan kusaidia upatikanaji wa walimu wa hisabati na sayansi na namna
ya kufundisha walimu wa masomo hayo nchini kama namna haraka ya kukabiliana na uhaba
mkubwa wa walimu wa masomo hayo nchini. Aidha, Tanzania imeiomba Japan kusaidia katika
uchapishaji wa vitabu vya sayansi na hisabati ili kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi
wa Tanzania anakuwa na nakala yake ya vitabu vya masomo hayo kama namna ya kuongeza
ubora wa elimu.
Tanzania imetoa maombi hayo kwa Japan Jumatatu, Juni 3, 2013,
wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipokutana
na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Ushirikiano na Misaada ya Kimataifa la
Japan (JICA) Dr. Akihiko Tanaka kwenye Hoteli ya Intercontinental Yokohama.
Rais
Kikwete amekuwa katika Japan kwa ziara ya siku saba ya kikazi akihudhuria Mkutano
wa Tano wa Tokyo Kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD V) ambao umefungwa asubuhi siku
ya Jumatatu. Rais amemwambia Dr. Tanaka kuwa moja ya changamoto kubwa zinazoikabili
sekta ya elimu ambayo imepanuka sana nchini katika miaka saba iliyopita ni ukosefu
wa walimu wa hisabati na sayansi, masomo ambayo ni msingi mkubwa wa maendeleo ya nchi.
“Kuna
mambo mawili ambayo nataka kuomba msaada wa JICA. Tuna tatizo kubwa la ukosefu wa
walimu wa hisabati na sayansi. Tuna uhaba wa kiasi cha walimu 26,000 wa hisabati na
sayansi lakini vyuo vyetu vyote vinaweza kutoa wahitimu 2,200 tu kwa mwaka. Hii ina
maana ili kuziba pengo hilo tutahitaji kiasi cha miaka 12 ambao ni muda mrefu sana.
Hivyo, tunaomba kuona namna JICA na Japan mnaweza kutusaidia katika hili,”amesema
Rais Kikwete na kuongeza:
“Mbali na ukosefu wa walimu wa hisabati na sayansi
ambalo sasa limekuwa jambo la dharura kabisa, napenda pia kuiomba Japan kupitia JICA
kuweza kuisaidia nchi yetu katika kuchapisha vitabu vya sayansi na hisabati kama namna
nyingine ya kuchangia jitihada za kuboresha elimu yetu,” Rais Kikwete amemwambia Dkt.
Tanaka.
Ameongeza Rais Kikwete: “Kwa hakika, tumekuwa tunapata msaada mkubwa
kutoka Serikali ya Marekani katika uchapishaji wa vitabu vya kiada kwa ajili ya shule
zetu za sekondari. Lakini bado mahitaji yetu ni makubwa na hivyo tunaomba kama mnaweza
mtusaidie katika eneo hili ambalo nalo ni la kuendeleza ubora wa elimu yetu.”
Rais
Kikwete amesema kuwa ni jambo la kufurahisha kuwa wakati wa mazungumzo yake na Waziri
Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Shinzo Abe amekubali kwamba atasaidia katika eneo hili la
sayansi na hisabati. Dr. Tanaka amemwambia Rais Kikwete kuwa JICA inatilia maanani
maendeleo ya sekta ya elimu na kuwa kati ya vijana 70 wa kujitolea wa Japan ambao
wanapelekwa Tanzania kila mwaka kiasi cha vijana 20 ni walimu wa hisabati na sayansi.
“Tunachoweza kusema ni kwamba tutaangalia kwa makini eneo hili na tutachukua hatua
stahiki katika kuwasaidia walimu wa hisabati na sayansi. Aidha, tutaangalia ni kwa
namna gani tunaweza kuongeza idadi ya walimu wa hisabati na sayansi miongoni mwa
vijana wa kujitolea wanaokwenda kufundisha katika shule za Tanzania kutoka Japan kila
mwaka.”