2013-06-04 15:26:03

Imetimia miaka hamsini tangu kutokea kifo cha Papa Yohane XX111


Jumatatu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Vatican, Papa Fransisko , alikutana na kikundi cha mahujaji kutoka Jimbo Katoliki la Bergamo Italia, kikiongozwa na Askofu Francesco Beschi, ambacho kilifanya hija Vatican, kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kutokea kifo cha mmoja wao, Mwenye Heri Papa Yohane XXIII,kwa jina jingine Angelo RONCALLI .

Katika hotuba yake, Papa Fransisko, alirejesha fikira zake wakati huo wa miaka 50 iliyopita ambako Mwenye Heri alifariki dunia, akisema kwa watu wa umri wake Papa Fransisko, bado wanazo kumbukumbu hai za siku hizo za mwisho wa maisha ya Papa Mwema, ambamo ujumbe wa kifo chake ulienea kwa haraka sana duniani kote na uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, kuwa mahali patakatifu na wazi kwa wote usiku na mchana, kutolea maombi yao kwa ajili ya Papa Mwema.
Papa Fransisko amemtaja hayati Papa Yohane XXIII kuwa, alitambuliwa na dunia kuwa ni Papa Mwema, Mchungaji na baba wa wote, kutokana na sifa zake kuwa ni unyenyekevu na amani, mambao mawili yaliyojijenga ndani mwake na kuwa mfumo wa tabia yake Askofu Mkuu RONCALLI. Unyenyekevu na amani ni ahadi yake ya tangu siku alipowekwa wakfu wa Askofu, kama jarida la Soul toleo la 13-17 Machi 1925 lilivyoeleza. .

Papa Fransisko amesema, Papa Yohane XX111, alitambuliwa kuwa mtu mwenye uwezo pia wa kuiwasilisha amani katika asili yake ya utulivu na kirafiki , amani aliyo onyesha kuwa nayo hata kabla ya kuchaguliwa kuwa Papa, akiitwa Baba Mwema.
Fadhila hii ya wema na amani, vilimwenzesha kujenga urafiki wa nguvu kila mahali na hasa wakati akiwa mwakilishi wa Papa, utume alioufanya kipindi cha karibia miongo mitatu, akijihusisha kwa karibu na mazingira yanayomzuguka na pia sehemu zingine za mbali zilizo sahaulika katika ulimwengu Katoliki. Alikuwa ni mfumaji hodari na fanisi katika ujenzi wa mahusiano na mkuzaji mzuri wa umoja na shikamano ndani na nje ya jumuiya ya Kanisa. Ndiye aliyeifungua milango ya mazungumzano kati ya Wakatoliki na Wakristo wa Makanisa mengine, na pia hata kwa wasiokuwa Wakristu, Wayahudi na Waislamu na waamini wa madhehebu mengine mengi, na watu wote wenye watu wa mapenzi mema.
Papa Fransisko amekiriā€ Kwa kweli, Papa Yohana XX111, aliipeleka amani kwa watu wote kwa hekima na busara , juhudi zilizotoa matunda ya kazi ya muda mrefu na changamoto nyingi binafsi na hivyo kukatika kwa maisha yake, kuliacha mengi ya kufuatiliwa juu ya maisha yake.
Papa Fransisko amemtaja Papa Mwema, kuwa mfano bora wa imani na fadhila ya kuigwa, si tu na watu wa Bergamo lakini kwa watu wa vizazi vyote vya Kikristu duniani.
Papa alitolea sala ili roho yake iendelee kuimarisha utafiti wa maisha yake na maandishi yake, lakini juu ya yote, kuiga utakatifu wake. Na kutoka mbinguni, aweze kuendelea kuliongoza kwa upendo Kanisa la Kristu ambalo yeye mwanyewe alilipenda katika maisha yake yote. Na pia ili aweze kupata toka kwa Mungu, zawadi ya miito mingi ya Upadre , miito ya kitawa na maisha ya kimisionari na pia kwa ajii ya maisha ya familia na uwajibikaji wa walei katika Kanisa na ulimwengu Ujumla.








All the contents on this site are copyrighted ©.