Huduma ya maji safi na salama pamoja na lishe bora zinahitaji mshikamano na uwajibikaji
wa pamoja!
Askofu mkuu Francis Chullikatt, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa,
akichangia mada kuhusu maendeleo endelevu na kwa namna ya pekee kipengele cha maji
na afya anasema kwamba, hizi ni sekta zinazohitaji kuwa na mshikamano na uwajibikaji
utakaowawezesha watu wengi zaidi kupata huduma hizi muhimu katika maisha ya mwanadamu.
Umefika wakati
kwa Jumuiya ya Kimataifa kuona umuhimu wa kutangaza kuwa mambo haya ni sehemu ya haki
msingi za binadamu, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kuendeleza na kuimarisha
haki msingi za binadamu na mafao ya wengi.
Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano
huu unabainisha kwamba, kwa miaka mingi umejitahidi kutoa ushawishi kwa Serikali na
Jumuiya ya Kimataifa kutambua kwamba, maji na huduma msingi za afya ni kati ya haki
msingi za binadamu lakini bila mafanikio, kwani Jumuiya ya Kimataifa bado inasita
kuonesha msimamo wake katika mambo haya. Lakini ukweli wa mambo unaonesha kwamba,
kuna zaidi ya watu millioni 800 ambao hawana huduma ya maji safi na salama, ingawa
maji ni sehemu ya uhai wa binadamu.
Hii ni changamoto pia kwa Jumuiya ya Kimataifa
kuhakikisha kwamba, watu wanapata huduma bora za afya kama sehemu ya utekelezaji wa
Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna
zaidi ya watu billioni 2.5 hawana huduma bora ya afya. Changamoto zote hizi ni fursa
makini kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha pekee katika mikutano yake ili
kubainisha mbinu mkakati utakaowawezesha watu wengi zaidi kupata haki zao msingi kwa
kuwa na uhakika wa maji safi na salama pamoja na huduma bora za afya.
Askofu
mkuu Chullikatt anafafanua kwamba, ili kuweza kufikia Malengo haya kuna haja kwa wadau
mbali mbali kutekeleza dhamana yao kwa vitendo badala ya kuendelea kutoa ahadi za
mikono mitupu! Jumuiya ya Kimataifa ibainishe ni kwa jinsi gani inaweza kutekeleza
haki hizi msingi, kwa kutambua kwamba, lengo ni kumhudumia kwanza mwanadamu licha
ya faida ionayoweza kupatikana katika huduma hii. Itakumbukwa kwamba, huduma ya maji
safi na salama inavuka mipaka ya nchi, jambo linalohitaji kwa namna ya pekee kujenga
na kuimarisha mshikamano wa kimataifa, kwa kusimamia rasilimali hii pamoja na kuwa
na matumizi bora kwa ajili ya mafao ya wengi.
Hapa kuna haja ya kuunda uongozi
madhubuti wa kikanda ili kuweza kukusanya nguvu ya pamoja, kwa kuzingatia: maendeleo,
usawa, busara na mshikamano wa kidugu katika kuratibu matumizi bora ya maji kama sehemu
ya mafao ya wengi. Wadau mbali mbali wanapaswa kushirikishwa ili kulinda na kudumisha
haki ya maji, inayopaswa kutumiwa kwa busara na kuepuka uwezekano wa kutumia maji
vibaya. Haki inapaswa kutumika kwa kutambua mtu, sheria na rasilimali fedha; mambo
yanayopaswa kusimamiwa na kanuni ya auni ili huduma hii iweze kutolewa kwa ufanisi
mkubwa.
Askofu mkuu Francis Chullikatt anabainisha kwamba, Malengo ya Maendeleo
ya Millenia yanapaswa kuwa ni kikolezo kikubwa cha maboresho ya maisha ya watu, sanjari
na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, bila kusahau huduma msingi za afya.
Jumuiya ya Kimataifa ifanye juhudi za makusudi ili kuhakikisha kwamba, watu wengi
wanapata huduma ya maji safi na salama, kwani hii ni sehemu ya haki zao msingi. Kuna
uhusiano mkubwa kati ya maji na usalama wa chakula kwa ajili ya: maisha, ustawi na
maendeleo ya binadamu. Rasilimali ya dunia itumike vyema ili kukidhi mahitaji ya kizazi
cha sasa na kile kijacho.