Hali ya chakula si shwari, kuna watu billioni mbili wanakabiliwa na baa la njaa duniani
Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja
wa Mataifa anasema kwamba, utapiamlo una gharama kubwa katika maisha ya kijamii pamoja
na maendeleo ya kiuchumi, kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe
ili kuhakikisha kwamba, utapiamlo unafutika katika uso wa dunia.
Katika kipindi
cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na mabadiliko makubwa, lakini bado kuna njia
ndefu ambayo Jumuiya ya Kimataifa haina budi kupitia ili kuhakikisha kwamba, tatizo
la utapiamlo linatoweka katika uso wa dunia. Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi mwaka
2012 kulikuwa na jumla ya watu millioni 870 waliokuwa wanakabiliwa na baa la njaa
duniani. Taarifa ya hali ya chakula kwa mwaka 2013 inaonesha kwamba, kuna watu billioni
mbili wanaoteseka kutokana na baa la njaa duniani, hali ambayo imepelekea afya ya
watu hawa kuwa hatarini.
Bwana Josè Graziano da Silva anasema, hali hii haiwezi
kukubalika duniani, kwani gharama na athari zake ni kubwa kwa uchumi wa Kitaifa na
Kimataifa. Hali ya maisha ya watu inaendelea kudorora sanjari na kuendelea kushamiri
kwa magonjwa nyemelezi yanayotokana na baa la njaa na utapiamlo. Kuna haja kwa wananchi
kupata lishe bora inatokana na kilimo cha kisasa kinachozingatia ubora wa mazao toka
pale yanapovumwa shambani hadi yanapomfikia mlaji.
Ili kupambana na tatizo
la utapiamlo kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza katika sekta ya kilimo; kudhibiti
upotevu wa chakula na kuongeza ubora wa lishe; walaji hawana budi kuwa na ufahamu
mpana zaidi wa chakula wanachokula pamoja na kuhakikisha kwamba, wanawake na watoto
wanapata chakula kwa wakati muafaka.