Japan kuwekeza Barani Afrika katika nishati na miundo mbinu ya usafirishaji
Serikali ya Japan imeahidi kuzipatia nchi za Kiafrika msaada wa Euro billioni 24.2
katika kila kipindi cha miaka mitano kama sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu
Barani Afrika.
Hayo yamebainishwa na Bwana Shinzo Abe, waziri mkuu wa Japan
wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Maendeleo Afrika, TICAD,
uliofunguliwa mwishoni mwa juma. Ni mkutano unaogharimiwa na Japan, Umoja wa Mataifa,
Benki ya Dunia na kwa mara ya kwanza Umoja wa Afrika umeshiriki pia.
Viongozi
wa Bara la Afrika wamepewa changamoto ya kuendeleza rasilimali watu, kufanya maboresho
makubwa katika sekta ya afya pamoja na kuongeza tija na uzalishaji kwenye sekta ya
kilimo. Haya ni maeneo makubwa yanayopaswa kufanyiwa kazi na viongozi wa Afrika kama
kichocheo cha maendeleo kwa kushirikisha sekta ya umma na ile ya binafsi. Bara la
Afrika linapaswa kuchukuliwa kuwa ni mdau mkubwa wa biashara na wala si tu mpokeaji
wa misaada kutoka nchi za nje.
Japan inatarajia kuwekeza zaidi katika masuala
ya nishati na usafirishaji Barani Afrika. Viongozi wa Afrika wamekumbushwa pia umuhimu
wa kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, amani na kwamba,
utulivu ni kigezo kikuu cha maendeleo Barani Afrika. Ni wajibu wa Afrika kwa kushirikiana
na Jumuiya ya Kimataifa kujitahidi kudhibiti vitendo vya uharamia vinavyokamisha usafirishaji
wa mizigo kwenye Bahari ya Hindi.