Kanisa halitaacha kutangaza Fumbo na Kashfa ya Msalaba
Kanisa ni Familia ya Mungu inayowajibika na kwamba, Wakristo hawana sababu ya kuogopa
Kashfa ya Fumbo la Msalaba. Watambue kwamba, Yesu Kristo ndiye Neno aliyefanyika mwili
na kukaa kwake Bikira Maria. Ni Mwana wa Mungu aliye hai na ni Mtakatifu wa Bwana.
Kanisa linatambua na kuliheshimu Fumbo la Umwilisho, ambalo kwa watu wengine ni Kashfa
ya Mwaka.
Ni sehemu ya mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe
Mosi, Juni 2013 aliyoyatoa kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Domus
Sanctae Marthae, kilichoko mjini Vatican. Kanisa linaendelea kutangaza Fumbo hili
kwa njia ya maisha na utume wake. Kanisa linaonesha kwa namna ya pekee, uwepo endelevu
wa Kristo miongoni mwa watu wake.
Kanisa linaungama na kukiri kwamba, Yesu
ni Mwana wa Mungu aliye hai. Kwa njia hii, Wakristo kama ilivyokuwa kwa Kristo mwenyewe
watakabiliana na madhulumu. Kwa hakika, Kashfa ya Msalaba ni sehemu ya maisha na utume
wa Kanisa. Ikumbukwe kwamba, Kanisa si ushirika wa kitamaduni, kidini wala kijamii,
bali ni Familia ya Kristo inayoendeleza utume wa Kristo hadi miisho ya dunia.
Baba
Mtakatifu Francisko anawaalika Wakristo kushuhudia kwa maneno na matendo yao kuhusu
ukweli wa Fumbo la Umwilisho: Kristo alizaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kutoka
katika wafu, limbuko lao waliolala katika usingizi wa amani. Kanisa kamwe halitaacha
kutangaza Fumbo na Kashfa ya Msalaba. Waamini wasimame kidete kutetea na kushuhudia
ukweli wa Fumbo hili.