2013-06-01 08:44:43

Injili ya Kristo inapaswa kutangazwa na watu wenye furaha, imani na matumaini kwa Kristo na Kanisa lake!


Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanashiriki ibada kwa moyo wa uchaji, imani, furaha na matumaini, kwani hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopaswa: kuheshimiwa, kuabudiwa na kutukuzwa na waja wake. Ni furaha inayobubujika kutoka katika undani wa mwamini anayeshikamana na Kristo katika hija ya maisha yake; ni furaha inayopata chimbuko lake katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani.

Baba Mtakatifu ameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu, Mama Kanisa alipokuwa anafanya kumbu kumbu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeth aliyekuwa amebahatika kupata mimba katika uzee wake. Hii ndiyo ile furaha iliyooneshwa na Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu walipompeleka mtoto Yesu kwa mara ya kwanza Hekaluni kadiri ya sheria. Ni furaha ambayo ni matunda ya uaminifu wa Mungu kwa waja wake wanaomkimbilia usiku na mchana.

Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuwaona vijana wakitekeleza sheria na wazee wakijiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza katika hija ya maisha yao hapa duniani. Roho Mtakatifu ni chemchemi ya furaha na uhuru wa kweli, kwani bila furaha waamini watagubikwa na huzuni pamoja na simanzi ya rohoni. Injili ya Kristo inapaswa kutangazwa na waamini wenye furaha, imani na matumaini kwa Kristo na Kanisa lake, tayari kuwashirikisha wengine sifa na utukufu wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujenga utamaduni wa kumsifu, kumtukuza, kumwabudu na kumwomba na kumshukuru Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Lakini, ukweli wa mambo ni kwamba, waamini wengi wamezoea kuomba tu, kiasi kwamba wanashindwa hata kushukuru baada ya kukirimiwa kile walichoomba! Waamini wajifunze kutoa muda wao katika maisha ya sala na ibada kwa Mwenyezi Mungu, kwani furaha ya kweli itawaweka huru.

Baba Mtakatifu mwishoni, amewaambia wafanyakazi wa Vatican kutoka kitengo cha ufundi, Sekretarieti ya Vatican walioandamana na viongozi wao kwamba, Kanisa ni kisima cha furaha ambayo inabubujika kutoka kwa Yesu Kristo. Waamini waonje na kuwaonjesha wengine furaha ya kweli wanapomtangaza na kumshuhudia Kristo katika maisha yao ya kila siku.







All the contents on this site are copyrighted ©.