2013-05-31 09:21:33

Yaliyojiri kwenye ziara ya Rais Kikwete nchini Japan


Japan imekubali kuangalia uwezekano wa kugharimia ukarabati na uboreshaji mkubwa wa Reli ya Kati na pia imekubali kuwa mbia mkuu katika kuiwezesha Tanzania kuleta mageuzi makubwa katika kilimo cha mpunga kwa nia ya kuzalisha mchele zaidi na kujitegemea kwa zao hilo muhimu la chakula.

Serikali ya Japan imeeleza msimamo huo wa kuisaidia Tanzania katika maeneo hayo baada ya kuombwa rasmi kufanya hivyo wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Tanzania na Japan kati ya Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Shinzo Abe.

Aidha, Japan imeombwa na kukubali kuangalia uwezekano wa kugharimia ujenzi wa reli mpya kutoka Tanzania kwenda nchi za Rwanda, Burundi na hatimaye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Tanzania pia imeiomba Japan kuwa mshirika kiongozi katika mageuzi ya kilimo cha mpunga katika Tanzania ili kuwezesha kuongeza usalama wa chakula na hasa wa mchele kwa Tanzania na majirani zake.

Tanzania vile vile imeiomba Serikali ya Japan kuyashawishi makampuni makubwa ya nchi hiyo kuwekeza katika uchumi wa Afrika kwa sababu Bara la Afrika linaendelea kuwa soko muhimu la bidhaa za viwandani za Japan. Maombi hayo yametolewa Alhamisi, Mei 30, 2013 na Rais Kikwete wakati alipokutana na kufanya mazungumzo rasmi na Mheshimiwa Abe, mjini Tokyo ikiwa sehemu ya shughuli za Rais Kikwete katika ziara ya kikazi ya siku saba katika Japan.

Katika mazungumzo hayo ofisini kwa Waziri Mkuu, Rais Kikwete ameiomba Japan kufikiria kuiunga mkono Tanzania kwa kugharimia ukarabati na uboreshaji wa Reli ya Kati kutoka reli nyembamba ya sasa kuwa reli ya kiwango kinachokubaliwa kimataifa. Aidha, Rais Kikwete ameiomba Japan kuangalia uwezekano wa kugharimia ujenzi wa reli mpya kutoka Isaka, Tanzania kwenda Kigali, Rwanda na hatimaye Burundi na DRC.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, reli yetu ya kati ni nzee sana na tunataka kuboresha reli yenyewe kwa kuibadilisha na kuifikisha kiwango cha kimataifa na pia kukarabati karakana zote muhimu za kuhudumia reli hiyo. Aidha, tunashirikiana na Rwanda, Burundi na DRC kujenga reli mpya kwa sababu nchi zote hizi zinategemea Bandari ya Dar es Salaam kupitisha mizigo yao,”

Ameongeza: “Tumekamilisha upembuzi yakinifu na michoro kwa msaada wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na kampuni moja ya Barrington Santa Fe ya
Marekani na sasa tunatafuta mbia wa kugharimia ujenzi wake.”

Kuhusu uboreshaji wa kilimo cha mpunga, Rais Kikwete amemwomba Waziri Mkuu Abe kuifanya Japan kuwa mbia kiongozi katika kilimo cha mpunga ili kuiwezesha Tanzania kujitegemea kwa mchele na hata kuweza kulisha nchi za jirani. “Katika kilimo, tunalenga kujitosheleza kwa mahindi na mchele. Tunao wabia wachache lakini tunataka Japan iwe mbia kiongozi kwa sababu ya uzoefu wetu katika kilimo cha mpunga. Tunahitaj kuongeza uzalishaji kwa sababu majirani zetu wanatutegemea.”

Kuhusu Serikali ya Japan kuyashawishi makampuni binafsi ya nchi hiyo
kuwekeza katika Afrika, Rais Kikwete amesema: “Biashara kati ya Japan na Afrika inaongezeka na uwekezaji unaongezeka, lakini tunaweza kufanya zaidi kwa sababu katika kila magari 10 kwenye barabara za Afrika tisa yanatoka Japan. Maduka ya vifaa vya elekroniki yamejaa vifaa na vyombo kutoka Japan – ziwe kamera, ziwe redio, ziwe televisheni lakini hayo makampuni mengi ya Japan yanawekeza katika Afrika.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Uwekezaji unatunufaisha sana katika Afrika.
Chukua mfano wa Kampuni ya Somitomo – imezalisha vyandarau milioni 30 pale Arusha na ni vyandarua hivyo ambavyo vimepunguza malaria katika
Afrika. Tanzania kwenye malaria imepungua kwa kiasi cha asilimia 60 kwa sababu ya uwekezaji huo.”

Rais pia ameiomba Serikali ya Japan kuisaidia kampuni hiyo ya Somitomo kuwekeza zaidi katika uzalishaji umeme. Kwa sasa kampuni hiyo inashirikiana na Serikali kuzalisha megawati 240 katika eneo la Kinyerezi, Dar Es Salaam.

Rais pia ameomba Japan kuongeza nafasi za shahada ya juu ya PHD katika kufundisha madaktari wa Tanzania na kusaidia kuongeza uwezo wa Tanzania katika matumizi ya mkongo wa taifa ambao Serikali iliujenga.



Japan yatangaza mabilioni kusaidia Tanzania

Japan imetangaza misaada na mikopo ya mabilioni ya fedha kusaidia
uchumi na maendeleo ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kugharamia uboreshaji wa miundombinu, ujenzi wa miradi ya barabara, ujenzi wa miradi ya maji, uanzishwaji wa skimu ndogo ndogo za umwagiliaji na uboreshaji wa kilimo cha mpunga.

Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Shinzo Abe ametangaza hatua hizo za kuunga mkono jitihada za maendeleo za Tanzania wakati alipokutana na kufanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete.

Viongozi hao wawili wamekutana ofisini kwa Mheshimiwa Abe, Alhamisi, Mei 30, 2013, mjini Tokyo kwenye siku ya pili ya ziara ya wiki moja ya Rais Kikwete katika Japan ambako miongoni mwa mambo mengine amealikwa kuhudhuria Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Kujadili Maendeleo ya Afrika wa Tokyo International Conference on African Development (TICAD – V) unaoanza Yokohama, mji wa pili kwa ukubwa katika Japan, Jumamosi, Juni Mosi hadi 3, 2013 na kuhudhuriwa na viongozi wa nchi za Afrika na washirika wa maendeleo wa Bara hilo.

Miongoni mwa miradi ambayo Japan imekubali kugharimia ambayo baadhi yake inaendelea kujengwa ama karibu inaanza kutekelezwa ni pamoja na Mradi wa Maji wa Mkoa wa Tabora, Mradi wa Kuboresha Usafiri katika Mkoa wa Dar Es Salaam ambao ni pamoja na kupanuliwa kwa Barabara ya Gerezani na Ujenzi wa Daraja Jipya kwenye barabara hiyo, Mradi wa Kuendeleza Kilimo cha Mpunga nchini na Mradi wa Awamu ya Pili ya Kuongeza Uwezo wa Serikali za Mitaa kwa Njia ya Mafunzo.

Miradi mipya ambayo Japan itagharimia ni pamoja na Mradi wa Kuendeleza Miundombinu, Mradi wa kujenga skimu ndogo za umwagiliaji, mradi wa ujenzi wa barabara ikiwa ni pamoja na kugharimia ujenzi wa barabara katika milango ya kimataifa ya Mara, Dodoma na Iringa na Mpango wa 10 wa Kuunga Jitihada za Kupunguza Umasikini.

Wakati wa mazumgumzo hayo, Waziri Mkuu Abe pia ametangaza kuwa Japan itagharamia ujenzi wa barabara za juu kwa juu (fly-overs) kwenye makutano ya barabara za TAZARA na Ubungo, ujenzi wa mtambo wa kuchakata umeme wa Kinyerezi ambako unatekelezwa kwa mpango wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPF).

Waziri Mkuu Abe pia ameitaka Tanzania na Japan kukamilisha “haraka iwezekanavyo” majadiliano ya kufikiwa kwa makubaliano ya kulinda uwekezaji kati ya nchi hizo mbili ili kufungua njia za uwekezaji zaidi katika uchumi wa Tanzania kutoka Japan, moja ya mataifa tajiri zaidi duniani.

Mheshimiwa Abe ameiomba Tanzania kuunga mkono jitihada za nchi hiyo kujiunga na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) chini ya mageuzi makubwa yanayotarajiwa kufanyika kwenye mfumo wa Umoja huo.

Rais Kikwete alijibu ombi hilo la Mheshimiwa Abe kwa kusema: “Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaunga mkono moja kwa moja jitihada za Japan kujiunga na Baraza la Usalama kama mwanachama mwenye kura ya turufu. Unajua msimamo wetu kuhusu jambo hili siku nyingi.”

Tanzania yaunga mkono ombi la Japan kuhusu Olimpiki

Tanzania imesema kuwa itaunga mkono ombi na jitihada za Jiji la Tokyo
katika Japan kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020. Msimamo huo wa Tanzania umetangazwa Alhamisi, Mei 30, 2013 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipokutana na kufanya mazungumzo rasmi na Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Shinzo Abe.

Katika mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwa Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Abe aliiomba Tanzania kuiunga mkono katika jitihada zake kadhaa za kimataifa ikiwa ni pamoja na kupata nafasi ya kuandaa Michezo ya Olimpiki mwaka 2020.

“Nina maombi mawili kwako Mheshimiwa Rais…moja ni kwamba Jiji la Tokyo ni moja ya miji ambayo inawania kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020. Tunaomba kuungwa mkono na Tanzania na tunaomba usaidie tuweze kuungwa mkono na Afrika,” Mheshimiwa Abe amemwambia Rais Kikwete.

Baada ya Mheshimiwa Abe kutoa ombi hilo, Rais Kikwete amesema: “Tutaiunga mkono nchi ya Japan na Jiji la Tokyo kuweza kuandaa Michezo ya Olimpiki mwaka 2020. Aidha, nataka kukuhakikishia kuwa tutatumia mahusiano yetu katika Afrika kuwezesha kuungwa mkono kwa ombi hilo la Japan.” Jiji la Tokyo ni miongoni mwa miji mitatu duniani ambayo imevuka hatua ya kwanza kutoka mji iliyoomba (applicant cities) na kuwa mji inayoweza kuandaa Michezo ya Olimpiki (candidate cities). Miji mingine miwili ni Madrid (Hispania) na Istambul (Uturuki).

Kabla ya hatua hiyo, miji mitano ikiwamo Tokyo, Madrid na Istambul
pamoja na Baku (Azerbaijan) na Doha (Qatar) ilikuwa imeomba kuandaa Michezo hiyo kabla ya idadi yao kupungua Mei 25, 2012. Uteuzi wa mwisho wa Mji ambao utandaa Michezo hiyo utatangazwa kufuatia kikao cha 125 cha Kamati ya Utendaji ya Kamati ya Olimpiki Duniani (IOC) kilichopangwa kufanyika Septemba 7, 2013 mjini Buenos Aires, Argentina. Tokyo mara ya mwisho iliandaa Michezo ya Olimpiki mwaka 1964.











All the contents on this site are copyrighted ©.