Unganeni na Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu! Mshirikisheni
Yesu: hofu na wasi wasi zilizomo mioyoni mwenu!
Askofu mkuu Paul Ruzoka, Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani, Baraza la Maaskofu Katoliki
anawaalika waamini kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi
Takatifu sanjari na kufanya Ibada ya Kuabudu, kama kielelezo cha mshikamano wa imani
na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ijayo kuanzia saa Saa 12:00 hadi Saa 1:00 kwa
saa za Afrika Mashariki.
Kama sehemu
ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu Francisko ataungana na Wakatoliki
sehemu mbali mbali za dunia kusali na kuabudu mbele ya Ekaristi Takatifu kwenye Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Askofu mkuu Paul Ruzoka anasema kwamba, hii
itakuwa ni nafasi kwa waamini kuweza kusali kwa ajili ya kuombea amani, upendo na
mshikamano. Waamini wasali ili Mwenyezi Mungu aweze kuwaepushia hatari zote, mashaka
na wasi wasi kwa kila mwamini mmoja mmoja na taifa katika ujumla wao.
Anawaalika
waamini kufuata utaratibu uliopangwa kwenye Majimbo husika, ili kuonesha mshikamano
na umoja katika Bwana mmoja na Imani moja, kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Ibada
hii ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Jumapili ijayo, tarehe 2 Juni 2013.