Mpendwa mwana wa Mungu, ninakualikeni tukatafakari pamoja Neno la Mungu leo ikiwa
ni sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Sherehe hii
ni kati ya sherehe za Bwana na huadhimishwa Dominika inayofuata mara baada ya sherehe
ya Utatu Mtakatifu. Ni sherehe ambayo ina uhusiano wa moja kwa moja na Alhamisi kuu
ambapo fumbo la Ekaristi Takatifu linawekwa katika Kanisa na Yesu Kristu mwenyewe.
Siku ya Alhamis Kuu hatukupata nafasi ya kusherehekea hasa kwa shangwe na
nderemo kwa kuwa tulikuwa tayari katika Juma Kuu, Juma la Mateso ya Bwana. Kumbe Mama
Kanisa anatujalia nafasi tena ya kusherehekea na kushangilia kwa vigelegele sherehe
hii hivi leo.
Ndiyo kusema katika sikukuu hii tunafanya ukumbusho wa Karamu
ya mwisho, ambapo Bwana alikula karamu hiyo pamoja na wanafunzi wake. Ni katika karamu
hiyo aliweka sakramenti ya Ekaristi na sakramenti ya Upadre. Mama Kanisa hufanya maandamano
katika siku hii ikiwa ni ishara ya ushuhuda wa imani akitangaza ukuu wa Mungu kwa
mataifa ambao hujidhihirisha kwa njia ya Ekaristi Takatifu. Ni ishara ya shukrani
kwa Mungu kwa ajili ya zawadi ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ekaristi
Takatifu ni chimbuko la Kanisa na hivi tunasherehekea na kushangilia zawadi ya Kanisa
pia kama Safina ya wokovu.
Mpendwa mwana wa Mungu, tunaposherehekea Sherehe
ya Mwili na Damu ya Bwana kwa shangwe Mama Kanisa atuwekea Neno la Bwana akitaka polepole
kutambua hicho tunachokisherehekea ni kitu cha thamani kuu. Mwinjili Luka anakuja
kwanza na maneno mawili Njaa na Jangwa. Kumbuka kunapotokea njaa katika maeneo yako,
natumai mahangaiko ni makuu hata zaidi ya vita ya silaha!
Njaa yaweza kuwa
chanzo cha mafarakano katika familia na imetokea hata mara kadhaa mababa wa familia
kukimbia na kuziacha familia zao. Kukosa chakula, yaani kuwa katika baa la njaa yawezekana
kutupa nafasi ya kufikiri juu ya thamani ya chakula na hivi tukiwanacho tukaweza kukitumia
vizuri. Tukitazama njaa kiroho inawezekana ikawa ni nafasi ya kuona pia mpango wa
Mungu kwetu.
Mpendwa msikilizaji, uthamani wa Ekaristi Takatifu waweza kueleweka
vema kupitia mang’amuzi ya njaa! Ebu fikiria mmoja akikwambia au akisema “sina muda
leo wa kwenda Misa au Misa inanichosha”. Mara moja huyu hana njaa na hajui thamani
ya Misa Takatifu, hajui thamani ya Ekaristi Takatifu. Katika hali ya namna hii hata
mmoja angesisitiza sheria haiwezekani kumfanya mmoja ashiriki Misa, yafaa kuwa na
njaa, njaa ya Neno la Mungu, njaa ya Misa, njaa ya Ekaristi Takatifu. Lakini pia yafaa
kujiuliza je ni njaa gani tunakuja nayo katika Misa?
Njaa ya kujisifu, ya
kuangalia, ya kusikiliza? Au ya kushiriki mafumbo ya Mungu? Yafaa kutafakari vema
aina ya njaa tunayopaswa kuwa nayo. Ni njaa ya kutaka kuchota neema kwa ajili ya kutekeleza
wito wa Bwana “nendeni duniani kote mkawafanye wote kuwa wanafunzi wangu”. Ni njaa
ya kutambua kuwa katika Msalaba, Bwana amemwaga Damu yake kwa ajili ya ulimwengu,
kumbe njaa ni kuwa na kiu ya kupeleka ujumbe wa upendo huo kwa mataifa.
Neno
la pili ni Jangwa, jaribu kufikiri juu ya jangwa yaani pale ambapo panasadikika kutokuwa
na maisha. Ni neno muhimu kwa ajili ya tafakari yetu maana ni hapo Bwana analeta maisha
kinyume na fikira za Mitume ambao waliona haiwezekani kufanya kitu zaidi ya kuwaaga
makutano. Bwana ni chanzo cha maisha pale ambapo hatuoni mbele wala nyuma.
Ni
Ekaristi Takatifu ambayo hutupa maisha katika ulimwengu wa leo ambao unaonekana kuwa
Jangwa. Machafuko, mauaji, siasa mpindisho zisizojari haki na usawa wa wananchi, zisizojali
huduma ya jamii ni vielelezo vya jangwa katika ulimwengu wetu. Bwana akisema heri
walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao, ataka daima kuleta amani itokayo
katika Ekaristi kwa njia ya unyenyekevu wa moyo.
Katika jangwa anapowapa chakula
anawaagiza Mitume wawaketishe watu katika safu ya watu hamsinihamsini akitaka kukuza
thamani ya maisha ya pamoja na kusaidiana na kushirikishana mapendo na ndiyo maana
ya kula pamoja. Bwana anatangaza kuwa Ekaristi ni sherehe ya pamoja, ni sherehe ya
ushirika, upendo, umoja na mshikamano wa dhati akitaka kuondoa Jangwa na upweke katika
maisha ya watu.
Mpendwa, Misa ndiyo maana yake hasa! Kwa nini wabaki nyumbani
wakati Bwana akuita ukakae na wenzio katika karamu yake? Natumai pia maandamano tufanyayo
yataka kuita mataifa wakatukuze ukuu wa Bwana na kwa njia ya kukaa pamoja. Maandamano
yataka watu waketi katika safu, wasafiri pamoja katika safu na hivi ondoleo la upweke
wa jangwani.
Mpendwa msikilizaji tunapopokea mwili na Damu ya Bwana, tunapokea
mwanga katika maisha yetu maana alisema mimi ni taa ya maisha yako, ni ukweli na uzima
kumbe pia twahuishwa na Bwana anayetaka toka maisha hayo tukafanye vivyo hivyo daima
mpaka ajapo. Anatualika kwa njia ya Ekaristi tuishi uhuru wa wana wa Mungu aliotupatia
Bwana (Lk. 4:18 na kuendelea).
Katika Injili tunayotafakari pia bado kuna
jambo la msingi na la wokovu. Baada ya kuwa wamekula mkate na samaki waliweza tena
kukusanya vikapu 12 vya mabaki. Hili mara moja latupa tumaini litokalo katika Bwana
kuwa Bwana aliye Ekaristi haishi kamwe, ni wa milele, hutosheleza mahitaji yetu yote
ya upendo jana, leo na daima (rejea maneno ya mbiu ya Yubileo Kuu ya Ukombozi mwaka
2000). Basi nasi twapaswa kuwa chemchemi ya mapendo na matumaini kwa wengine na kwa
Kanisa la Kristu.
Mpendwa msikilizaji tunaposherehekea tunapaswa kufikiri kwa
undani sana nini maana ya fumbo hili kuu na mwisho lazima, tafakari yetu imalizikie
katika neno moja “PENDANENI KAMA NILIVYOWAPENDA NINYI”. Ninawatakieni furaha tele
nikiwakumbusha fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu hadi nitakaporudi” Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.