Kanisa Katoliki linapenda kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini ili kujenga
na kuimarisha urafiki, udugu na haki msingi za binadamu!
Padre Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya
Kidini yuko nchini Uturuki ili kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya
Wakristo na Waislam. Huu ni mwendelezo wa mkataba uliotiwa sahihi kunako mwaka 2002
kati ya Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini na Serikali ya Uturuki ili kuendeleza
uhusiano mwema kati ya waamini wa dini hizi mbili.
Kwa pamoja waamini wanaalikwa
kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kuabudu; Mafundisho tanzu ya imani zao,
uhuru wa dhamiri pamoja na kukuza malezi na majiundo ya maisha ya kiroho na malezi
kwa vijana. Ni mchakato unaopania kwa namna ya pekee, kuendeleza ushirikiano wa karibu
katika sekta ya elimu kwa kuweka utaratibu na kanuni ambazo zitasaidia vyuo na taasisi
za kidini kuweza kushirikiana.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na
sita, katika hija yake ya kichungaji nchini Uturuki kunako tarehe 28 Novemba 2006
alibainisha umuhimu wa nchi ya Uturuki katika maisha na utume wa Kanisa, kwani hapa
ni mahali ambapo Jumuiya nyingi za Kanisa la mwanzo zilianzishwa; ni nchi ambayo ina
utamaduni wa hali ya juu wa dini ya Kiislam unaojionesha katika: Fasihi, Sanaa pamoja
na Taasisi mbali mbali zilizopo.
Itakumbukwa kwamba, Mwenyeheri Yohane Paulo
wa Pili alitembelea nchini Uturuki kunako mwaka 1979. Majadiliano ya kidini ni muhimu
sana miongoni mwa Wakristo na Waislam, ili kujenga na kudumisha urafiki; haki, amani,
upendo na mshikamano miongoni mwa Jamii. Huu ndio msimamo unaofanyiwa kazi pia na
Baba Mtakatifu Francisko, kama alivyobainisha wakati alipokutana na viongozi wawakilishi
wa dini mbali mbali hapo tarehe 20 Machi 2013.