Tahadhari la tishio la mlipuko wa ugonjwa wa kupooza (Polio)
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania, imepokea taarifa mnamo tarehe 22
Mei 2013 kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni, (WHO) ya kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa
wa kupooza (Polio) katika Wilaya ya Fafi nchini Kenya. Mpaka sasa kuna mgonjwa mmoja
bila kifo.
Ugonjwa wa Polio ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi
vijulikanavyo kama “Polio Virus”. Ugonjwa huu unaathiri misuli na mfumo wa fahamu
hivyo kusabisha kupooza kwa viungo hasa miguu na hata kifo. Ulemavu huu ukishajitokeza
huwa ni wa kudumu. Waathirika wakuu wa ugonjwa huu ni watoto hasa walio na umri chini
ya miaka mitano. Hata hivyo ugonjwa huu unazuilika kwa chanjo ya Polio ambayo ni salama
na inatolewa bure na Serikali katika vituo vyote vya huduma ya afya. Mtoto aliyepata
chanjo ya Polio anakuwa amekingwa na ugonjwa wa Polio kwa maisha yake yote.
Kutokana
na taarifa hiyo ya kutoka nchini jirani ya Kenya, baadhi ya mikoa ina uwezekano mkubwa
wa kupata maambukizo ya ugonjwa huo kufuatia ushauri wa kitaalam. Aidha, mikoa hii
mingine inapakana na nchi jirani ya Kenya na mingine ina mapungufu yaliyopo katika
hali ya chanjo ya Polio. Mikoa hii ni pamoja na Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Arusha,
Manyara, Kilimanjaro, Mara na Mwanza.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:
Kutoa
taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya.
Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika
Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipaka
Kufuatilia kwa karibu hali ya chanjo mikoani
na wilayani hususan ya Polio hususani iliyo katika hatari ya maambukizi
Kuhamasisha
watoto ambao hawajakamlisha ratiba yao ya chanjo hususani ya Polio au ambao hawajapata
ya chanjo hii waweze kwenda vituo vya karibu vya afya vya kutolea chanjo
Wizara
inapenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa Viongozi na Watendaji wa ngazi zote kutoa
ushirikiano ili kuhakikisha kila mtoto mlengwa anapata chanjo ya Polio. Aidha Wizara
inatoa rai kwa wadau wetu, taasisi za dini, taasisi zinazofanya kazi katika jamii
na vyombo mbalimbali kuhamasisha watu wapeleke watoto wao kwenye vituo vya huduma
wakapewe chanjo hii muhimu. Chanjo hii ni salama na inatolewa bila malipo.
Wananchi
wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara wanapoona
au kupata taarifa ya mtoto yoyote anayepata ulemavu wa ghafla pasipo sababu yoyote.
Mtoto huyo apelekwe katika kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na hatua za haraka.
Imetolewa
na; Nsachris Mwamwaaja Kitengo cha Mawasiliano Serikalini 30/05/2013