Maaskofu Katoliki Madagascar wanawataka wananchi wa Madagascar kusimama kidete kulinda
na kutetea haki, amani na upatanisho wa kitaifa!
Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa
Mwaka kwa kujadili masuala kadhaa yanayogusa maisha na utume wa Kanisa nchini Madagascar,
lakini kwa namna ya pekee nchi yao inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa
kufanyika hapo tarehe 24 Julai 2013.
Baraza la Maaskofu linawaalika waamini
na watu wote wenye mapenzi mema kuiombea Madagascar ambayo kwa miaka ya hivi karibuni
imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbali mbali, kiasi cha kuwakosesha watu amani, furaha
na matumaini ya maisha. Wanawaomba waamini kushirikiana kwa pamoja kwa ajili ya kuombea
amani na ufanisi katika mchakato wa uchaguzi mkuu, ili uweze kuwa huru, wa haki na
uwazi bila kudanganya watu, kwani huu unaweza kuwa ni mwanzo wa mgogoro na machafuko
ya kisiasa.
Maaskofu wanawaalika wananchi wa Madagascar kushiriki kikamilifu
katika mchakato wa uchaguzi mkuu nchini humo ili kuhakikisha kwamba, wanawachagua
viongozi adili watakaosimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, utu na heshima
ya binadamu; viongozi ambao wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa umoja na mshikamano
wa kitaifa; viongozi ambao wataanzisha mchakato wa upatanisho ili kuganga madonda
na utengano ambayo yamekuwa ni kizingiti kikubwa cha maendeleo na ustawi wa wananchi
wa Madagascar.
Wananchi watataka kuona kwamba, wale watakaochaguliwa wana
sifa za kuongoza, ni watu wanaoonesha uzalendo kwa nchi yao; viongozi ambao wako tayari
kutumia vyema rasilimali na utajiri wa nchi kwa ajili ya maendeleo ya wengi na wala
si kwa ajili ya kujinufaisha wao binafsi, ndugu, jamaa na marafiki zao kama ambavyo
historia inabainisha.
Maaskofu wa Madagascar wanasikitika kusema kwamba, licha
utajiri mkubwa ambao nchi yao imebahatika kuwa nao, lakini bado wananchi wake wanaendelea
kuogelea katika: umaskini wa hali na kipato; magonjwa na ujinga; kinzani na migawanyiko
hata ndani ya familia zenyewe; rushwa na ufisadi wa mali ya umma pamoja na ukosefu
wa misingi ya haki, amani na usalama kwa raia na mali zao. Mataifa ya kigeni yamekuwa
yakiingilia mambo ya ndani ya nchi ya Magagascar, hali inayoonesha kwa namna ya pekee
ukosefu wa utashi wa kisiasa na uzalendo.
Baraza la Maaskofu Katoliki Madagscar,
linawaalika waamini na wananchi wote wenye mapenzi mema kuanza mchakato wa upatanisho
na mshikamano wa kitaifa kwa kutambua kwamba, Kanisa kama Mama na Mwalimu, linalo
jukumu na dhamana ya kukemea yale yote yanayotaka kuvuruga na kuwagawa wananchi wa
Madagascar, ili kuenzi na kudumisha utu na heshima ya binadamu; mafao ya wengi pamoja
na ustawi wa wananchi wote wa Madagascar.
Baraza la Maaskofu Katoliki Madagscar
linaliwaalika vijana kwa namna ya pekee kuwa ni wajenzi wa misingi ya haki, amani,
upendo na upatanisho wa kweli na kamwe wasitumiwe na wanasiasa ucharwa kuvuruga amani
nchini humo. Vijana wanachangamotishwa kuwa ni vyombo vya haki na amani na wadau wakuu
wa maendeleo endelevu. Maaskofu wanawakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi
mema kusali kwa ajili ya kuombea haki na amani kwa kutambua kwamba, haki ni msingi
wa amani.