Msalaba ni kielelezo cha upendo, huruma na hekima ya Mungu kwa mwanadamu. Ni alama
ya ushindi na matumaini, umoja na mshikamano wa dhati.
Ni maneno
ya Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni wakati akishirikisha
mchango wa mawazo yake kwenye mkutano wa Makanisa Ulimwenguni ulifanyika hivi karibuni
kwa kupania kujenga na kuimarisha mshikamano wa dhati na Wakristo wanaoishi huko Mashariki
ya Kati, ambao kwa sasa wanakabiliana na hali ngumu ya maisha.
Dr. Tveit amewakumbusha
wajumbe wa mkutano huo kwamba, kila Mkristo anapaswa kuubeba vyema Msalaba wake na
kumfuasa Kristo, lakini pia kama Jumuiya ya Wafuasi wa Kristo wanachangamotishwa na
Mama Kanisa kusaidiana kubebeana Misalaba, kama kielelezo cha upendo na mshikamano
wa Wafuasi wa Kristo huko Mashariki ya kati. Mkutano huu ulioanza hapo tarehe 21 hadi
tarehe 25 Mei, 2013 ulikuwa umeandaliwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana
na Baraza la Makanisa Mashariki ya Kati. Mkutano huu umefanyika mjini Beirut, huko
Lebanon.
Dr. Tveit anasema, mshikamano maana yake ni kuonesha kwamba, kama
Wakristo wanathamini zawadi ya maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura
na mfano wa Mungu na kwamba, wanapania kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kwa
ajili ya ustawi na mafao ya wengi kwa sasa na kwa siku za usoni. Mshikamano wa Kikristo
ni muhimu sana huko Mashariki ya Kati ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbali
mbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa haki, amani na autulivu unaopelekea kinzani na
migogoro ya kijamii.
Huu ni mwaliko kwa waamini wa dini na madhehebu mbali
mbali kufanya kazi kwa pamoja ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maendeleo
endelevu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa miaka kadhaa limekuwa likijishughulisha
na mchakato unaopania kujenga na kuimarisha misingi ya haki na amani huko Mashariki
ya Kati, hususan kati ya Palestina na Israeli.
Baraza la Makanisa kwa kushirikiana
na Makanisa mbali mbali huko Mashariki ya Kati linapania pamoja na mambo mengine kudumisha
amani pamoja na haki msingi za binadamu; kukomesha uvamizi ili uhuru uweze kutawala
na vita kusitishwa.
Ni wajibu na dhamana ya Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha
kwamba, inatoa suluhu ya kisiasa katika mgogoro kati ya Israeli na Palestina. Kushindwa
kufanya hivyo, kumepelekea vitendo vya utekaji nyara kuongezeka huko Mashariki ya
Kati na kwamba, vita inayoendelea nchini Syria ina madhara makubwa kwa wananchi wasiokuwa
na hatia. Mkutano huu umehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Makanisa huko Mashariki
ya Kati.