Parokia ya Laisamis, Jimbo Katoliki la Marsabit, Kenya, inaadhimisha Jubilee ya Miaka
50 tangu ilipoanzishwa!
Askofu mstaafu Ambrogio Ravasi, Jumapili iliyopita, tarehe 26 Mei 2013 ameongoza umati
mkubwa wa waamini na marafiki wa Parokia ya Laisamis, Jimbo Katoliki la Marsabit,
Kenya kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu ilipofunguliwa, ikiwa ni Parokia ya kwanza
Jimboni humo.
Askofu mstaafu Ravasi amewaambia waamini na watu wenye mapenzi
mema waliokuwa wamehudhuria katika Ibada hii ya Misa Takatifu kwamba, uwepo wao ni
matunda ya imani shirikishi yanayoonesha hija ya Familia ya Mungu nchini Kenya. Hii
ni Parokia iliyoanzishwa miezi minne kabla ya Kenya kujipatia uhuru wake kutoka kwa
Mwingereza. Parokia hii kwa mara ya kwanza ilihudumiwa na Mapadre Luigi Graiff na
Mario Valli kutoka katika Shirika la Wamissionari wa Consolata.
Hii ni Parokia
ambayo imedhamiria kujitegemea na kulitegema Jimbo kwa kutumia rasilimali watu na
mali inayopatikana Parokiani hapo kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Licha ya
Parokia hii kufungwa kwa takribani mwaka mmoja na kuendelea kupata huduma kutoka kwa
Wamissionari wa Consolata, waamini wameendelea kubaki imara katika imani yao kwa Kristo
na Kanisa lake bila kuyumbishwa wala kutetereka, matendo makuu ya Mungu.
Parokia
ya Laisamis ina jumla ya vigango vitatu na katika kipindi cha miaka 50 iliyopita imekuwa
ni chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Wamissionari wa Consolata walihudumia
Parokia hii tangu ilipoanzishwa hadi mwaka 1990 walipoikabidhi kwa Jimbo Katoliki
la Marsabit, nchini Kenya.