2013-05-29 09:29:08

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani: Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kuanzia saa 11 hadi saa 12:00 Jioni, Jumapili tarehe 2 Juni 2013


Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa linalohamasisha Uinjilishaji Mpya anasema, hadi sasa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yanaendelea kushika kasi kwa kuonesha utajiri mkubwa unaofumbatwa katika matukio mbali mbali yanayoratibiwa na Kanisa la kiulimwengu hata pia kwa Makanisa mahalia. Hadi sasa kuna zaidi ya mahujaji millioni 4,300,000 walioshiriki katika sala, tafakari na ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake hapa mjini Roma.

Yote haya ni matukio yanayoonesha ukomavu wa kiimani katika hija ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Jumapili ijayo, kuanzia saa 11: 00 hadi Saa 12:00 za jioni kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Kanisa zima katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu inaongozwa na kauli mbiu "Bwana mmoja, Imani moja".

Hili litakuwa ni tukio la kihistoria kuwahi kufanyika ndani ya Kanisa Katoliki, kwani Makanisa makuu ya Majimbo yote Katoliki duniani, Parokia, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, pamoja na nyumba za kitawa, kwa muda wa saa nzima, wataungana kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Itakumbukwa kwamba, Ekaristi Takatifu ni chanzo na kiini cha maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa Mlango wa Imani, anawachangamotisha waamini kuhakikisha kwamba, wanalishwa kwa Neno la Mungu na kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Chakula cha uzima wa milele. Ibada ya Misa Takatifu inachukua umuhimu wa pekee kabisa katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu iliyoanzishwa rasmi kunako mwaka 1246, Mwaka ambao Kanisa pia lilitangaza rasmi Siku kuu ya Ekaristi Takatifu. Ibada hii imeendelea kupendwa na waamini wengi kushiriki kiasi kwamba, kuna baadhi ya Makanisa ambayo yana Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa muda wote!

Askofu mkuu Rino Fisichella anabainisha kwamba, Jumapili jioni, Waamini wataungana na Baba Mtakatifu Francisko kila watu kadiri ya mazingira na changamoto wanazokabiliana nazo. Kuna baadhi ya waamini Makanisa yao makuu yameharibiwa na tetemeko la ardhi, hao wanasema, watakuwa pamoja na Baba Mtakatifu kwa kuabudu Ekaristi Takatifu katika eneo la wazi. Baadhi ya majimbo yamebainisha kwamba, muda uliopangwa kwao ni usiku, lakini hata hivyo, wataungana na Baba Mtakatifu ili kukesha na Kuabudu Ekaristi Takatifu.

Kuna baadhi ya maeneo ya dunia, hayana umeme wa kuaminika, lakini hata wao wanasema, wako pamoja ili kumuunga mkono Baba Mtakatifu Francisko, kama kielelezo cha imani katika matendo. Licha ya mvua, hofu na wasi wasi kadhaa, lakini Maaskofu wanasema, watasimama kidete kuhakikisha kwamba, Ibada hii ambayo ni tukio la kihistoria katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani linafanikiwa.

Askofu mkuu Rino Fisichella anasema kwamba, muda huu wa saa nzima, kuanzia saa 11:00 hadi saa 12:00 jioni, utakuwa ni muda utakaosheheni: Sala, Tafakari ya Kina na Mshikamano wa Imani miongoni mwa Waamini wa Kanisa Katoliki. Baadhi ya Majimbo yana desturi ya kufanya Maandamano ya Ekaristi Takatifu mara baada ya Kuabudu. Majimbo hayo yataendelea na utaratibu waliojiwekea, kwani yote haya ni kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu anayeendelea kufanya hija na waja wake katika historia na matukio mbali mbali ya maisha.

Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu Jumapili ijayo, anapenda kukazia nia zifuatazo: Kanisa ambalo limetawanyika sehemu mbali mbali za dunia, linaungana pamoja kwa ajili ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, changamoto ya kujenga utamaduni wa kusikiliza Neno la Mungu kwa umakini mkubwa pamoja na kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Kanisa kwa kuwa aminifu kwa Neno la Mungu linalolitangaza, watu waweze kupata wokovu na hatimaye, kushiriki katika maisha ya uzima wa milele. Kanisa lieendelee kuwa ni chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu pamoja na kuonesha mshikamano na wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali, ili wote hawa waonje furaha na utulivu wa ndani.

Katika Ibada hii ya Kuabudu, Baba Mtakatifu Francisko, anawaalika waamini kuwakumbuka wale wote ambao wametumbukizwa katika utumwa mamboleo, wanaoishi katika machafuko ya vita, migogoro na kinzani za kijamii; waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya; pamoja na wale wote wanaoteseka katika hali ya ukimya; wote hawa wapate msaada na huduma kutoka kwa Mama Kanisa ambaye anaukumbatia Msalaba wa Kristo.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwakumbuka na kuwaombea wale wote wanaoteseka kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa; wasiokuwa na fursa za ajira, wazee, wahamiaji na wakimbizi; wasiokuwa na makazi, wafungwa na wale wote wanaotengwa kutokana na sababu mbali mbali; waonje na kufarijika kwa uwepo wa Kristo anayewakirimia matumaini mapya na kwamba, utu wao unapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.