Kanisa ni familia ya Mungu inayotumwa kutangaza Injili hadi miisho ya dunia!
Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake, Jumatano, tarehe 29 Mei 2013, baada
ya kuhitimisha mfufulizo wa Katekesi kuhusu Kanuni ya Imani, kama sehemu ya Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, ameanza Katekesi Mpya kuhusu Fumbo la Maisha na Utume wa Kanisa,
mintarafu Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kwa namna ya pekee, Baba
Mtakatifu Francsiko ameanza kwa kuchambua Kanisa kama Familia ya Mungu.
Kama
inavyooneshwa katika mfano wa Baba mwenye huruma, Mwenyezi Mungu anawataka watu wote
kuishi na kudumu katika pendo lake ili kuweza kushiriki maisha yake. Kanisa ni sehemu
muhimu sana ya Mpango wa Mungu; kwani mwanadamu ameumbwa ili kumfahamu na kumpenda
Mwenyezi Mungu licha ya uwepo wa dhambi miongoni mwa wanadamu, lakini Mwenyezi Mungu
anaendelea kuwaalika ili waweze kutubu na kumrudia tena.
Baba Mtakatifu anasema,
katika utimilifu wa nyakati, Mwenyezi Mungu alimtuma Mwanaye wa Pekee kuja hapa ulimwenguni
ili kuanzisha Agano Jipya na la Milele na binadamu wote kwa njia ya sadaka yale pale
Msalabani. Kanisa ni tunda la upendo unaopatanisha, kwa njia ya maji na damu iliyobubujika
kutoka ubavuni mwa Kristo, pale walipomchoma mkuki ubavuni.
Katika Sherehe
ya Pentekoste, Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume kwa kuwakirimia nguvu ya kutangaza
Injili ya Upendo wa Kristo hadi miisho ya dunia. Baba Mtakatifu anasema, kamwe Kristo
hawezi kutenganishwa na Kanisa lake, ambalo ameliwezesha kuwa ni Familia kubwa ya
Watoto wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuamsha tena ndani mwao
ari na moyo wa kulipenda Kanisa, ili kweli liweze kuwa ni Familia ya Mungu, m ahali
ambapo kila mtu anajisikia kwamba, anakaribishwa, anaeleweka na kupendwa.
Baba
Mtakatifu anaendelea kuwaalika waamini kulipenda na kuliombea Kanisa ili hatimaye,
liweze kuwa kweli ni chombo cha huruma, umoja na upendo wa Mungu kwa jirani.
Ni
mwaliko pia wa kumwilisha imani kama Familia ya Mungu inayowajibika, kwa kuonesha
upendo kwa Familia. Anawaombea Roho Mtakatifu ili awasaidie kutenda mema katika maisha
yao ya kila siku. Anawataka waamini kuhakikisha kwamba, Jumuiya zao za Kikristo zinakuwa
ni alama ya ukarimu; huruma na upendo wa Mungu kwa jirani.
Anawataka vijana
kuwapenda, kuwaheshimu na kuwaombea wazazi wao kwani wao ni chemchemi ya maisha na
zawadi kubwa inayowawajibisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Anawataka kujitoa kimasomaso
kushiriki katika maisha na utume wa Familia: kiroho na kimwili. Anawataka waamini
wanaofanya hija ya maisha yao ya kiroho kwenye makaburi ya Mitume, kuimarisha imani
yao kwa Kristo na Kanisa lake na kwa namna ya pekee wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha
Mwaka wa Imani.
Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko, anawaalika waamini na
watu wenye mapenzi mema kushiriki pamoja naye katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi
Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, kuanzia majira ya Saa
Moja Kamili Usiku, Alhamisi, tarehe 30 Mei 2013 na kuhitimishwa kwa Baraka Kuu ya
Ekaristi Takatifu kwenye Kanisa la Bikira Maria Mkuu lililoko mjini Roma. Baba Mtakatifu
anasema, Ibada ya Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha imani na amana muhimu sana katika
maisha ya Kanisa na binadamu kwa ujumla wake.