2013-05-29 09:37:04

Kanisa linaendelea kuwekeza katika tunu msingi za maisha ya kifamilia!


Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia anasema, Kanisa linaendelea kuwekeza katika majiundo makini ya tunu msingi za maisha ya kifamilia, ili familia ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla, kwani upendo wa binadamu kamwe hauwezi kuwa mkamilifu, unahitaji kuboreshwa siku hadi siku.

Familia ni shule ya upendo, mahali ambapo wanafamilia wanajifunza kuishi kwa pamoja, wakishirikiana na kushirikishana karama na vipaji walivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao. Ni mahali ambapo wanafamilia wanatambua tofauti zao kuwa ni utajiri mkubwa unawasaidia kujenga na kuimarisha: haki, amani, upendo na mshikamano ndani ya familia. Wanafamilia wanapaswa kutambua tofauti iliyopo kati yao na kwamba, utofauti huu si chanzo cha kinzani wala mikingamo, bali ni mwaliko wa kushirikiana na kukamilishana kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Sayansi na maadili yawasaidie wanafamilia kutambua wajibu na dhamana yao na kwa namna ya pekee, wajielekeze kuwaelimisha watoto wao katika maadili na utu wema, kwani kimsingi wazazi na walezi ndio waalimu wa kwanza wa watoto wao.

Askofu mkuu Jean Laffitte, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Familia anabainisha kwamba, uwepo wa wazazi wote wawili yaani Baba na Mama ni jambo muhimu sana katika makuzi na ukomavu wa watoto. Wazazi hawa wawili kwa kushirikiana kwa pamoja wanaweza kurithisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, kiutu na kiimani kwa watoto wao na kwamba, dhamana na utume wao hauna mbadala.

Mama ni kimbilio na usalama wa watoto; Baba kwa upande wake ni kielelezo cha sheria na utaratibu wa maisha. Lakini wote hawa wanaunganishwa na kifungo cha upendo na malezi kwa watoto wao, ili waweze kukua na kukomaa na hatimaye, kufikia utu uzima. Hata hivyo ikumbukwe kwamba, upendo huu bado unasimikwa katika vionjo vya kibinadamu kumbe, si mkamilifu unapaswa kuboreshwa siku hadi siku. Licha ya mapungufu haya, anasema Askofu mkuu Jean Laffitte, mtoto anaweza kupata yale mambo ya msingi.

Semina na Makongamano yanayoendeshwa na Baraza la Kipapa kwenye Makao yake Makuu kwa wakati huu yanagusia kwa namna ya pekee: dhamana na nafasi ya wazazi; familia tenge; upendo usiokuwa mkamilifu na wazazi wanapokuwa kinyume cha matarajio ya watoto wao! Wadau wanaendelea kushirikisha utajiri unaofumbatwa katika tofauti za maisha ndani ya familia; madhara ya familia tenge na uhusiano na watoto wao.

Mama Kanisa anatambua na kuthamini Familia kama shule ya utakatifu, haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli, kila mtu anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake, ili familia iendelee kupeta, licha ya kinzani na changamoto zinazoendelea kujitokeza kwa wakati huu.







All the contents on this site are copyrighted ©.