Ratiba elekezi kwa Maadhimisho ya Kiliturujia yatakayoendeshwa na Baba Mtakatifu Francisko
Mei hadi Julai 2013
Monsinyo Guido Marini, Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa, hivi karibuni ametoa
ratiba elekezi ya Maadhimisho ya Ibada mbali mbali zinazotarajiwa kuongozwa na Baba
Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Mwezi Mei hadi Julai, 2013. 00:03:46:42
Baba Mtakatifu Francisko baada ya kutembelea na kusali na Familia ya Mungu,
Parokia ya Watakatifu Elizabeth na Zakaria, iliyoko mjini Roma alitoa Sakramenti ya
Komunio ya kwanza kwa watoto 16 na watu wazima 28, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika
Jumapili iliyopita, tarehe 26 Mei 2013. Kanisa pia lilikuwa linaadhimisha Sherehe
ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kujiandaa kwa matukio
mengine ya kikanisa kama ifuatavyo:
Tarehe 30 Mei 2013, Kanisa mjini Vatican
linaadhimisha Siku kuu ya Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa
kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano
lililoko mjini Roma, ambalo kimsingi ni Makao Makuu ya Jimbo kuu la Roma, kuanzia
saa 1:00 Usiku na baadaye kufuatiwa na Maandamano makubwa ya Ekaristi Takatifu kupitia
mitaa kadhaa ya Mji wa Roma hadi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu.
Hapo
waamini watapata nafasi ya kuabudu Ekaristi Takatifu na baadaye, Papa atatoa baraka
ya Ekaristi takatifu. Maandamano ya Ekaristi Takatifu kuzunguka mitaa na viunga vya
mji wa Roma, waamini wakiwa wameshikilia mishumaa inayowaka imekuwa na mvuto na ushuhuda
wa imani kwa Kristo anayefanya hija ya maisha na wafuasi wake hadi utilimifu wa nyakati.
Jumapili, tarehe 2 Juni 2013 kuanzia saa 11:00 hadi saa 12:00 jioni kwa saa
za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, akiungana
na waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watakaokuwa wanaadhimisha Ibada hii
kwa wakati huo huo, kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Jumapili,
tarehe 16 Juni 2013, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya Maadhimisho ya
Siku ya Injili ya Uhai, changamoto kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kusimama
kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni
mwa mama yake hadi pale Mwenyezi Mungu anapomwita mja wake kutoka katika ulimwengu
huu ili kuweza kuungana naye katika maisha ya uzima wa milele.
Jumamosi, tarehe
29 Juni 2013, Kanisa litakuwa linaadhimisha Siku kuu ya Miamba wa Imani: Mitume Petro
na Paulo, walioyamimina maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia imani yao
kwa Kristo na Kanisa lake.
Hii ni siku ambayo Baba Mtakatifu ataadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu kwa mara ya kwanza na Maaskofu wakuu wapya walioteuliwa hivi
karibuni sanjari na kuwavisha Pallio Takatifu; Ibada itakayoadhimishwa kwenye Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 3:30 asubuhi. Pallio takatifu ni
alama ya umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Na kwa Ibada hii, Baba
Mtakatifu atakuwa anafunga kirago cha Maadhimisho ya Ibada kwa Mwezi Juni 2013.
Jumapili,
tarehe 7 Julai 2013, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa
Takatifu kwa ajili ya Majandokasisi na Wanovisi kutoka katika Seminari na nyumba za
malezi. Haya ni Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa Waseminari na Wanovisi, wanaopaswa
kutambua kwamba, Mama Kanisa ana matumaini makubwa kwao kwa sasa na kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya Kanisa la Kristo kwa siku za usoni.
Naam, kuanzia Jumatatu
tarehe 22 Julai hadi tarehe 29 Julai 2013, Baba Mtakatifu Francisko atakuwa afanya
hija yake ya kwanza ya kichungaji nchini Brazil, ili kushiriki na umati wa vijana
kutoka sehemu mbali mbali za dunia katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani,
inayoongozwa na kauli mbiu ”Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi”.
Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo: 28:19.
Kama ilivyo ada, Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican itakula nawe sahani moja ili kuhakikisha kwamba, inakujuvya kwa kina
na mapana yale yatakayojiri katika Maadhimisho haya. Ukiwa na haraka zako, unaweza
kutembelea katika mtandao wa Radio Vatican kwa anuani ifuatayo: