2013-05-28 08:45:02

Ondoeni vikwazo na vizingiti vinavyowakwamisha katika kumfuasa Kristo kwenye njia ya uzima!


Mwenyezi Mungu ndiye Bwana wa nyakati na anawaalika watu wote kumfuasa bila kuweka masharti wala vizingiti na kwamba, utajiri kisiwe ni kisingizio cha kutoweza kumfuasa Yesu Kristo kikamilifu kwa kumtolea ushuhuda wa upendo wa dhati, ili hatimaye, kuweza kurithi maisha ya uzima wa milele. Umwilishaji wa Amri za Mungu ni jambo la muhimu sana katika maisha ya mwanadamu, lakini mwamini anapaswa kuwa makini zaidi ili kuondokana na mambo yale ambayo yanaweza kuwa ni kikwazo katika ufuasi wa Kristo.

Ni sehemu ya mahubiri iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu asubuhi, kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae kilichoko mjini Vatican. Anasema, kila mtu ana utajiri ambao amekirimiwa na Mwenyezi Mungu, lakini kwa bahati mbaya, utajiri kama huu umekuwa ni chanzo cha majonzi na kikwazo cha ufuasi kwa Kristo. Kila mwamini anachangamotishwa na Kristo kuchunguza dhamiri yake kuona ni kwa jinsi gani ambavyo utajiri wake umekuwa ni kikwazo cha kumfuasa Kristo katika njia ya uzima wa milele.

Watu wengi wanataka raha mustarehe pamoja na kuwa na maisha bora; mambo ambayo wakati mwingine yamekuwa ni kizingiti katika maamuzi ya maisha ya kifamilia, kiasi kwamba, hata watoto ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu wameonekana kuwa ni mzigo usiobebeka na matokeo yake, watu wengi wanashindwa kujongea kwa Yesu. Baadhi ya watu wanataka mambo mpito! Lakini Mwenyezi Mungu ana mpango rasmi kwa kila mwanadamu. Huu ni mpango endelevu ambao kamwe hauwezi kupitwa na nyakati.

Huwezi kumjaribu Kristo anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa kutaka kuwa Padre wa kipindi cha mpito au mwanandoa wa mkataba! Pale unapokwisha basi, Upadre au ndoa inavunjika. Muda na utajiri ni vikwazo vikuu katika kumfuasa Yesu. Baba Mtakatifu anawapongeza Wamissionari waliojitosa kimaso maso kuhubiri Injili ya Kristo sehemu mbali mbali za dunia bila ya kuweka kizingiti katika maisha na utume wao kwa Kristo na Kanisa lake. Kuna wanandoa ambao pia wameshikamana hadi pale kifo kilipowatenganisha, huu ndio ufuasi wa Kristo pasi na masharti.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumwomba Yesu Kristo ili aweze kuwakirimia ujasiri utakaowafanya kujitosa kimasomaso bila ya woga ili kumfuasa Kristo bila ya kurudi nyuma. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na viongozi na wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi katika sekta ya afya; wafanyakazi wa Idara ya Uchumi pamoja na wahudumu wa Zahanati ya Watoto wadogo ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.