Imarisheni tunu msingi za maisha ya kifamilia ili kukabiliana na changamoto za utandawazi
na maendeleo ya sayansi na teknolojia!
Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia amehitimisha hija
ya kichungaji nchini Argentina na Chile ambako alikwenda kuimarisha mchakato unaopania
kudumisha tunu msingi za maisha ya familia pamoja na kuishukuru Familia ya Mungu nchini
Argentina, kwa kulizawadia Kanisa la kiulimwengu, Baba Mtakatifu Francisko ambaye
kwa sasa anaendelea kulipyaisha Kanisa kwa ari na msukumo mpya katika maisha na utume
wake.
Akiwa nchini Argentina na Chile, Askofu mkuu Paglia alipata fursa ya
kutoa mhadhara kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki Argentina, kama sehemu ya kumbu kumbu
ya Maadhimisho ya Miaka 30 tangu Umoja wa Mataifa ulipotoa Tamko la Haki Msingi za
Familia.
Anasema, Familia inakabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbali
mbali katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kuna sera
na mwelekeo wa kisiasa ambao unataka kufisha na kudhohofisha tunu bora za maisha ya
kifamilia mintarafu mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.
Askofu mkuu
Paglia akiwa nchini Argentina amekutana na kuzungumza na familia ambazo hivi karibuni
ziliathirika kutokana na mafuriko makubwa. Baraza la Kipapa la Familia, kwa kuguswa
na hali hii, liliamua kuunga mkono jitihada zilizokuwa zinafanyika kwa ajili ya kusaidia
familia ili ziweze kupata tena mahali pazuri pa kuishi. Ilikuwa ni fursa ya kukutana
na kuzungumza na viongozi wa shughuli za kifamilia kutoka Shirikisho la Mabaraza ya
Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini.
Askofu Paglia akiwa nchini Chile ambayo
waamini wake wengi wana ibada kwa Bikira Maria wa Mlima Karmeli, aliwataka wasomi
na wanazuoni nchini humo kuibua mbinu mkakati utakaoiwezesha familia kupewa kipaumbele
cha kwanza miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Anasema, kimsingi Familia inafumbatwa
katika upendo wa dhati kati ya Bwana na Bibi, kama njia ya kukamilishana, wakiwa tayari
kushiriki katika mpango wa kazi ya Uumbaji na malezi kwa watoto wao ambao ni zawadi
safi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Askofu mkuu Paglia alipata pia fursa ya kuzungumza
na kujadiliana na vijana wa kizazi kipya kuhusu umuhimu wa ndoa na maisha ya kifamilia
kadiri ya mpango wa Mungu. Amewataka vijana kusimama kidete na kamwe wasikubali kuyumbishwa
na athari za utandawazi zinazotaka kumong'onyoa tunu msingi za kimaadili na utu wema!