2013-05-27 08:45:32

Papa ajionea mwenyewe maisha na utume wa Parokia zilizoko pembezoni mwa Mji! Atoa Mahubiri kwa mtindo wa maswali na majibu!


Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Jumapili iliyopita, tarehe 26 Mei 2013 amefanya hija ya kichungaji kwenye Parokia ya Mtakatifu Elizabeth na Zakaria iliyoko pembezoni mwa Mji wa Roma.

Baba Mtakatifu amefanya mahubiri yake kwa njia ya maswali na majibu kwa watoto 44 waliopokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza katika maisha yao. Amezungumzia jinsi ambavyo Bikira Maria akisukumwa na upendo kwa jirani alivyokwenda kwa haraka kumsaidia binadamu yake Elizabeth aliyekuwa ni mjamzito.

Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa yuko daima tayari kuwasaidia wale wote wanaokimbilia ulinzi na maombezi yake; ni alama ya usalama, imani na matumaini kwa wote wanaomwita. Anawasaidia waamini kuweza kumfahamu Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa njia ya Yesu Kristo, ili kuyafahamu maisha na kazi za Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Mwenyezi Mungu ni Muumbaji; amegawanyika katika Nafsi Tatu: Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Mungu Mwana ni Mkombozi anayewapenda na kuwafundisha wafuasi wake Neno la Mungu. Ndiye aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Mungu Roho Mtakatifu analitakatifuza Kanisa.

Baba Mtakatifu amewaambia watoto waliopokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza kwamba, Yesu Kristo katika Fumbo la Ekaristi Takatifu anawaonjesha upendo wake na kuwakirimia nguvu mioyoni mwao. Anawaongoza na kuwalinda hadi waweze kuufikia uzima wa milele. Hii ilikuwa ni Katekesi ambayo watoto waliopokea Komunyo ya kwanza hawataweza kuisahau kwa urahisi katika maisha yao.

Mara baada ya Misa Takatifu, Papa Francisko amewashukuru waamini wa Parokia ya Mtakatifu Elizabeth na Zakaria kwa ukarimu waliomwonesha. Amempongeza Padre Alfred, Paroko ambaye anatimiza miaka 29 ya Ukasisi wake. Amefurahi kuona Parokia ambayo imechangamka na kuwa na watoto wengi. Amewataka kuendelea kusonga mbele kwa imani na matumaini, daima wakimkumbuka katika sala zao.







All the contents on this site are copyrighted ©.