Mwenyezi Mungu bado anaendelea kufanya hija na waja wake!
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Sherehe za Fumbo
la Utatu Mtakatifu aliwaambia waamini na mahujaji waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu petro mjini Vatican kwamba, alikuwa anamshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kumwezesha kwa mara ya kwanza kufanya hija ya kichungaji katika Parokia
ya Jimbo kuu la Roma. Anawaomba waamini kuendelea kumsindikiza katika utume wake kwa
njia ya Sala.
Baba Mtakatifu anasema, Adhimisho la Mwanga wa Fumbo la Pasaka
linapyaisha kila mwaka ile furaha inayobubujika kutoka katika imani, kwa kutambua
kwamba, Mungu ni upendo na asili ya maisha; ni upendo ambao umejionesha kwa namna
ya pekee kwa njia ya mateso na kifo cha Kristo Msalabani na kwamba, ni upendo huo
unaomwezesha pia Roho Mtakatifu kuendelea kumgeuza mwanadamu na kuumba upya sura ya
nchi.
Kwa kutambua kwamba, Mungu ni upendo, mwamini anachangamotishwa kupenda
na kujitoa kwa ajili ya jirani zake, kama alivyofanya Yesu anayeendelea kufanya hija
pamoja na wafuasi wake katika njia ya maisha. Fumbo la Utatu Mtakatifu ni ile sura
ya Mwenyezi Mungu iliyofunuliwa na Yesu na kuahidiwa kwa Roho Mtakatifu. Mwenyezi
Mungu katika Agano la Kale ametembea na Waisraeli na Yesu anaendeleza hija hii akiwa
pamoja na wafuasi wake na kwamba, amewaahidia Roho Mtakatifu atakayewafundisha ukweli
wote; anawaongoza na kuwakirimia mawazo mazuri. Kanisa linaadhimisha Fumbo la Utatu
Mtakatifu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, anayewapenda na kutaka waingie katika utawala
wake ambao ni uzima wa milele.
Baba Mtakatifu aliwaweka waamini wote chini
ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria aliyeonesha unyenyekevu wa hali ya juu, kiasi
kwamba, sasa amekwisha ingia katika hija ya uzima wa milele na utukufu wa Fumbo la
Utatu Mtakatifu. Bikira Maria, Mama wa Kanisa ni kielelezo makini cha matumaini katika
hija ya maisha ya imani. Ni Mama Mfariji.