2013-05-27 09:07:42

Mwenyeheri Padre Pino Puglisi ni shahidi na mfiadini; mchungaji mahiri aliyejitoa bila ya kujibakiza, ili kupandikiza mbegu ya msamaha na upatanisho!


Kardinali Paolo Romeo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Palermo, Italia, Jumamosi, tarehe 25 Mei 2013 amemtangaza Padre Pino Puglisi kuwa Mwenyeheri, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa watu kutoka ndani na nje ya Italia.

Padre Pino Puglisi ni shahidi mfiadini, mchungaji wa kweli aliyetekeleza utume na dhamana yake bila ya kujibakiza, kiasi hata cha kumwaga damu yake. Ni Padre aliyepandikiza mbegu ya msamaha na upatanisho; huyu ndiye aliyeuwawa kinyama na Kikundi cha Mafia, kunako tarehe 15 Septemba 1993, wakati alipokuwa anaadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu alipozaliwa.

Alikuwa ni Paroko wa Brancaccio, Jimbo kuu la Palermo. Mchakato wa kumtangaza kuwa Mwenyeheri ulianzishwa na Kardinali Salvatore de Giorgi kunako tarehe 15 Septemba 1999 na hatimaye kuidhinishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita tarehe 28 Juni 2012. Mwenyeheri Pino Puglisi atakuwa anakumbukwa Kiliturujia kila mwaka ifikapo tarehe 21 Oktoba. Kardinali Salvatore de Giorgi, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Palermo ndiye aliyemwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada hii ya Misa Takatifu.

Katika mahubiri yake, Kardinali Paolo Romeo amesema, Mwenyeheri Padre Pino Puglisi alikuwa ni mtu mwenye tabasamu la kukata na shoka, tabasamu ambalo liliwaunganisha watu na Kanisa limetambua kwamba, kifo chake ni kutokana na chuki za kidini “In odium fidei”, mfano wa kuigwa na waamini wengine katika kusimamia mambo msingi ya imani bila ya kuteteleka wala kuyumbishwa.

Ni mbegu ya mtu aliyejitoa kimasomaso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake ambayo imezikwa ardhini na sasa Kanisa linavuna matunda ya utakatifu wa maisha. Huu ndio mwaliko kwa familia na vijana wa kizazi kipya katika hija ya maisha ya miito yao ndani ya Kanisa. Waamini watambue kwamba, maisha yao yana thamani kubwa, wanayo paswa kuwashirikisha na kuwamegea wengine. Ni kielelezo makini cha Mapadre katika maisha na utume wao.

Katika eneo la Brancaccio lililokuwa linatawaliwa na kumilikiwa kwa kiasi kikubwa na Kikundi cha Mafia, Padre Puglisi, alisimama kidete kuwainjilisha watu bila woga, tangu wakati huo, maisha yake yalianza kuwa hatarini na kifo chake ni ujumbe makini kwamba, ukarimu wa mwenyeheri hautasahaulika kamwe. Maneno na matendo ya Padre Puglisi yaliwatia kichefu chefu watesi wake kiasi cha kuwanyima raha! Ni maneno yaliyokuwa yanagusa dhamiri na undani wao wa maisha. Alijitoa kweli kweli kwa ajili ya vijana, maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii. Alijenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini.

Kardinali Paolo Romeo anaendelea kusema kwamba, kwa mambo ya msingi, Padre Pino Puglisi hakuwa na mzaha! Alisimama kidete kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya mwanadamu vinapewa kipaumbele cha kwanza, sheria na utawala bora vinazingatiwa; akawaonesha waamini na wananchi waliomzunguka kwamba, walikuwa ni wa Mungu Baba kama Baba yao na wala si vinginevyo. Ni Mungu Baba, asili ya wema na ukarimu wote; anayewahimiza watu kujitoa kwa ajili ya mafao ya jirani zao.

Kikundi cha Mafia kimekuwa ni chanzo cha dhuluma na mauaji ya kinyama kwa viongozi na wananchi wengi wa Italia. Ni watu wanaomkana Mungu ambaye ni asili ya wema, upendo na maisha yote; wanakumbatia utamaduni wa kifo, chuki na hali ya kulipizana kisasi. Bado maneno ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili yanaendelea kusikika katika mioyo ya wananchi wa Palermo, tubuni, vinginevyo siku moja, mtakiona cha mtema kuni!

Wakati huo huo, Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican katika ujumbe wake kwenye Maadhimisho haya anasema, kwa mfano wa Padre Puglisi, shahidi wa imani na upendo elimishi hasa miongoni mwa vijana, aendelee kuwa ni mfano bora wa kuigwa na waamini pamoja na Jamii kwa ujumla kwa kutoa majibu muafaka mintarafu wito kutoka kwa Kristo. Ibada ya kumtangaza Padre Puglisi kuwa ni Mwenyeheri ni sherehe na ushuhuda kwa Kanisa nchini Italia.








All the contents on this site are copyrighted ©.