2013-05-27 08:19:31

Mauaji ya Mwenyeheri Giuseppe Puglisi ni kielelezo cha ushindi wa Kristo Mfufuka, changamoto kwa Kikundi cha Mafia kutubu na kumwongekea Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, aliwakumbusha waamini kwamba, Jumamosi, tarehe 25 Mei 2013, Kanisa limemtangaza Padre Giuseppe Puglisi, Mfiadini aliyeuwawa kikatili na Kikundi cha Mafia kuwa Mwenyeheri. Ni Padre aliyejipambanua kutokana na shughuli zake za kichungaji, hasa miongoni mwa vijana.

Aliwafundisha tunu msingi za maisha mintarafu Injili ya Kristo, akawatoa kwenye vurugu za maisha, jambo ambalo liliwafanya watesi wake kumfutilia mbali kutoka katika uso wa dunia, wakadhani kwamba, wameshinda, lakini kwa njia ya Kristo Mfufuka, Padre Puglisi ndiye aliyeshinda.

Baba Mtakatifu Francisko ameyapeleka mawazo yake kwa watu mbali mbali wanaonyanyaswa na kudhulumiwa na kikundi cha Mafia kiasi kwamba, wanajikuta wakitumbukizwa katika utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye kwa ajili ya kuwaombea Mafia ili waweze kutubu na kuongoka kwani vitendo wanavyovifanya ni kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu. Kanisa linamshukuru Mungu kwa mfano na ushuhuda makini uliotolewa na Padre Giuseppe Puglisi; kwa hakika ni mfano bora wa kuigwa.

Baba Mtakatifu alitambua uwepo wa Kikundi kikubwa cha waamini kutoka China, waliokuwa wamefika mjini Roma kwa ajili ya kusali kwa ajili ya kuiombea nchi yao chini ya usimamizi wa Bikira Maria Msaada wa Wakristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.