Yaliojiri katika uzinduzi wa Sinodi ya Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania
Tarehe 19 Mei, 2013 Kanisa liliadhimisha Sherehe ya Pentekoste. Kwa wanajimbo la Musoma,
siku hii ilikuwa na upekee zaidi. Ilikuwa ni siku ya Uzinduzi Rasmi wa Sinodi ya Jimbo.
Uzinduzi huo ulifanyika kwa adhimisho la Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Michael
Msonganzila wa Jimbo la Musoma na kuhudhuriwa kwa wingi na Mapadre, Watawa na Waamini
toka pembe zote za Jimbo.
Adhimisho la Misa Takatifu lililoanza majira ya saa
4:00 asubuhi, lilifanyika katika Viwanja vya Matumaini Katika Vijana, vinavyopakana
na Kanisa Kuu la Jimbo. Hii ilikuwa ni Misa pekee iliyoadhimishwa kwa Jimbo zima siku
hiyo ili kuwapa nafasi mapadre wote, watawa na waamini jimboni kushiriki pamoja katika
tukio hilo muhimu sana katika historia ya Jimbo. Watu walianza kukusanyika viwanjani
hapo kuanzia saa moja asubuhi na kufikia majira ya saa tatu sehemu kubwa ya viwanja
hivyo ilikuwa tayari imeshafurika watu. Wengi walifika kivikundi: kiparokia na vyama
vya kitume wakiwa na sare zao.
Maandamano yalitanguliwa na tukio la Askofu
kugonga kengele ya Kanisa Kuu la Jimbo. Tendo hili lilimaanisha kuwa yeye akiwa mchungaji
mkuu wa Jimbo anaitisha kusanyiko la Kijimbo kwa ajili ya kuadhimisha Sinodi na anawaalika
kondoo wake kushiriki. Kisha maandamano yalianza kuelekea eneo la Ibada, eneo lililopampwa
kifani kwa rangi nyekundu na nyeupe kuakisi sherehe ya Kiliturujia ya Pentekoste iliyoadhimishwa
siku hiyo.
Mwanzoni mwa Misa, Padre Robert Luvakubandi, Paroko wa Parokia ya
Musoma Mjini alipata nafasi ya kutoa neno la utangulizi na kumkaribisha Baba Askofu
kuongoza adhimisho.
Katika neno lake, Pd. Luvakubandi ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Kamati ya Maandalizi ya Sinodi alimjulisha Baba Askofu kuwa shughuli nzima ya maandalizi
imekamilika. “Shughuli hiyo imechukua takribani miezi kumi tangu Julai mwaka jana
ulipounda Kamati Kuu ya Maandalizi ya Sinodi” alieleza Pd. Luvakubandi. Alifafanua
kuwa maandalizi hayo yalijumuisha vikao vya Kamati kupanga ratiba na picha nzima Maadhimisho
yatakavyokuwa, kukusanya maoni toka kwa wanajimbo, kuandaa Sala ya Sinodi, kuandaa
Kauli Mbiu na wajumbe wa vikao. “Maandalizi hayo” aliendelea kufafanua “yalijumlisha
pia semina elekezi iliyotolewa tarehe 21 na 22 Januari kwa wajumbe wote wa sinodi
uliowaalika wewe Baba Askofu”.
Katika adhimisho hilo la Misa, lililofanyika
kwa uchangamfu na ushiriki hai wa waamini wote katika nyimbo na matendo mengine ya
kiibada, Askofu aliwaapisha wajumbe wote wa vikao vya Sinodi waliokuwapo. Wajumbe
hawa ni Mapadre wote wanaofanya utume Jimboni Musoma, wawakilishi wa mashirika ya
Kitawa yaliyoko Jimboni na wawakilishi kutoka parokia na taasisi zote za Jimbo. Kiapo
walichokula, kwa sehemu kubwa, kilikuwa ni ungamo la Imani. Hii ni kwa sababu maadhimisho
ya Sinodi ni tendo la Imani na kwa namna ya pekee yanafanyika katika Mwaka wa Imani.
Mahubiri
ya Askofu Msonganzila katika Ibada hii ya Misa, yaligusa dhamira zote za siku hiyo,
yaani Sherehe ya Pentekoste, Sikukuu ya Walei na Uzinduzi wa Sinodi. “Wapendwa wanafamilia
ya Mungu wa Jimbo la Musoma” ndivyo alivyoanza Askofu na kuendelea “leo ni Sherehe
ya Pentekoste; sherehe ambayo inahitimisha Kipindi cha Pasaka… Kwa namna ya pekee
leo tunasherehekea utimilifu wa Ahadi ya Bwana Yesu kwa Mitume kabla ya kupaa kwake
mbinguni, yaani ujio wa Roho Mtakatifu. Pia tunakumbuka kuzaliwa kwa Kanisa na mwanzo
wa Utume wa Kanisa. Siku hii pia imewekwa na Kanisa kama sherehe ya Waamini walei”.
Askofu alieleza kuwa kwa wanajimbo la Musoma kusanyiko kubwa la wanajimbo
katika Sherehe hii katika Viwanja vya Matumaini katika Vijana lina umuhimu wa kipekee
katika historia ya Jimbo kwa sababu ni kusanyiko pia la Uzinduzi wa Sinodi. “Kwa sababu
hii twaweza kupaita mahala hapa Viwanja vya Matumaini katika Sinodi!”
Masomo
ya liturjia ya siku yalitoka Mdo. 2:1 – 11; 1Kor. 12:3b – 7, 12 – 13; na Yn. 20:19
– 23. Akifanua masomo hayo, Askofu alieleza kuwa Roho Mtakatifu waliyempokea Mitume,
aliwapa ujasiri mkubwa wa kulihubiri Neno la Mungu. Roho huyo alikuwa ndio sababu
ya Umoja na Uelewano uliokuwa umepotea kati ya Mataifa kwa sababu ya dhambi.
Aliendelea
na kusema kuwa Roho Mtakatifu ndiye msingi wa karama na huduma mbalimbali katika Kanisa
na ndiye anayefanya karama hizo zilete faida na umoja katika Kanisa. Aliongeza kuwa
Roho huyu aliyefanya kazi ya kuwaunganisha mitume na Yesu, sasa anawaunganisha watu
na Mungu kwa kuwaondolea dhambi zao. Na matunda yake makuu ni Amani kati ya Mungu
na watu.
“Roho huyu tunayempokea katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa”
alisisitiza “anatuwajibisha tumshuhudie kwa maneno na maisha yetu”. Alionya kuwa “Tunapomtambua
Roho Mtakatifu kati yetu, tunalazimika tusiwe na Majivuno na Dharau kwa wengine. Roho
tuliyepewa si kwa ajili ya utukufu wetu wenyewe bali ni kwa ajili ya kuujenga mwili
wa Yesu yaani Kanisa”
Katika mahubiri hayo Baba Askofu aliwaalika waamini wote
kumpa Roho Mtakatifu nafasi katika maisha yao ili atende kazi ndani yao. “Jenga mazingira
ya Roho Mtakatifu kutenda kazi ndani yako” alisisitiza.
Baba Askofu alihitimisha
mahubiri yake kwa kueleza ratiba na mada kuu za Vikao vya Sinodi. Mintarafu ratiba,
alieleza kuwa maadhimisho yote ya Sinodi yanategemea kuchukua takribani Miaka Miwili
hadi kuhitimishwa kwake tarehe 03 Oktoba 2014. Na ndani ya kipindi hicho matukio makuu
yafuatayo yataadhimishwa. Baada ya Uzinduzi kutakuwa na vikao vikuu vine. Kikao cha
Kwanza (03 – 07 Juni 2013), kikao cha Pili (09 – 13 Desemba 2013), kikao cha Tatu
(28 Aprili – 02 Mei 2014) na kikao cha nne (04 – 08 Agosti 2014).
Mada kuu
zitakazojadiliwa ni mosi; UINJILISHAJI WA IMANI NA CHANGAMOTO ZA NYAKATI ZETU, MIITO
NA CHANGAMOTO ZA WAKATI, pili; LITURJIA YA KANISA NA MAISHA YA SAKRAMENTI, tatu; UTUME
WA HAKI, AMANI NA UPATANISHO na nne; MAENDELEO NA KUJITEGEMEA. Kisha hayo Askofu alitoa
tamko kuwa Sinodi Imezinduliwa.
Ilikuwa ni siku nzuri na iliyosubiriwa kwa
hamu sana na wanajimbo wote. Ikizingatiwa kuwa hii ndiyo Sinodi ya Kwanza ya Jimbo
wengi wana hamasa ya kuwa washiriki katika tukio hili kubwa la kihistoria katika Jimbo.
Kote jimboni sasa salamu inayotawala ni: Sinodi Musoma: Imani na Matendo, ndiyo salamu
ya Sinodi.
Baadhi ya waamini waliopata nafasi ya kuzungumza na mwandishi wa
makala hii hawakusita kuonesha hisia zao za furaha na matumaini makubwa kuwa adhimisho
la Sinodi litafanikiwa kuliongezea jimbo uhai na ustawi.
SINODI MUSOMA: IMANI
NA MATENDO. Waweza kupata habari zaidi kuhusu Sinodi kwa kutembelea blogu:
au kwa kujiunga ukurasa wa Facebook:
Imeandaliwa na Padre Alfred Kwene, Jimbo
Katoliki la Musoma.