Papa Francisko, Jumapili anatembelea Parokia ya Elizabeth na Zakaria pamoja na kutoa
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa waamini 44
Katika Maadhimisho ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Papa Francisko, Jumapili tarehe 26
Mei 2013 anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji kwenye Parokia ya Watakatifu Elizabeth
na Zakaria, iliyoko mjini Roma. Ibada ya Misa Takatifu inatarajiwa kuanza hapo saa
3:30 kwa saa za Ulaya. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, Papa Francisko atato pia
Sakramenti ya Ekaristi kwa Wakristo 44. Kati yao kuna watoto 16 na watu wazima 28.
Hii
ni hija ya kwanza ya Baba Mtakatifu Francisko kufanya kama Askofu wa Jimbo kuu la
Roma tangu alipochaguliwa kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni Parokia yenye
Wakristo 15,000. Parokia ilianzishwa hapo tarehe 28 Oktoba 1985 kwa hati iliyotolewa
na Kardinali Ugo Poletti. Kuanzishwa kwa Parokia hii kulitoa fursa kwa Waamini kuweza
kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa heshima zaidi kwani hapo mwanzoni walilazimika kutumia
ukumbi kama mahali pa Ibada. Tangu wakati huo, Parokia imeendelea kucharuka katika
maendeleo ya watu: kiroho na kimwili.
Tarehe 26 Oktoba 1997, Mwenyeheri Yohane
Paulo wa Pili alitembelea Parokiani hapo. Ushirikiano kati ya Waamini na Viongozi
wao wa Kanisa umefanikisha maendeleo yote yaliyokwisha kupatikana katika Kipindi cha
Miaka 25 iliyopita.